1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

WFP- Upungufu wa misaada utazusha Baa la Njaa Afghanistan

27 Machi 2023

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kupungua kwa ufadhili wa mataifa wahisani wa Afghanistan kunaweza kuisukuma sehemu ya taifa hilo katika baa la njaa kwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4PJEP
Afghanistan Zerstörung von Drogenanbauflächen in Provinz Badghis im Westen
Picha: press office Badghis Province Police

Sehemu kubwa ya misaada ya kiutu ilisitishwa na mataifa wahisani baada ya Taliban kuchukua hatamu ya uongozi wa Taliban mwaka 2021. Misaada hiyo ilisaidia sana kuepusha Afghanistan kwa njaa wakati huo, lakini kwa sasa kitisho kimeonekana kuongezeka zaidi.

Mkurugenzi wa WFP kwa Afghanistan, Hsiao-Wei Lee ameliambia shirika la habari la Uingereza-Reuters kwamba kutokana na unafuu wa awali kulikuwa na uwezekano wa kujiepusha na janga la njaa lakini kama hakutakuwa na uwezo wa kurejesha tena ufadhili huo, basi upo uwezekano wa kushuhudia hali ngumu zaidi.

Kwa sasa WFP ina upungufu wa dola milioni 93 katika kipindi hiki cha miezi ya Machi na Aprili, hali ambayo imepunguza mgao wa misaada ya kiutu kwa takribani Waafghanistan milioni 4 ikiwa sawa na kiwango cha asilimia 50 ya kile wanachohitaji.

Watu wengine milioni 9 watashindwa kufikiwa na msaada wa chakula mwezi ujao ikiwa ufadhili hautafika nchini humo katika majuma yajayo.

Misimamo ya Taliban ni chanzo cha kupungua misaada

Taarifa hiyo  ya WFP ni mojawapo ya ishara za kwanza muhimu baada ya hapo awali maafisa wa Jumuiya ya  Kimataifa kuonya kuwa kuongezeka kwa mipango ya kushughulikiwa kwa  dharura na Jumuiya ya Kimataifa na changamoto za hali ya kiuchumi, pamoja na  tendo la Taliban kuweka vikwazo kwa wanawake, vinaweza kusababisha wafadhili kujiondoa.

Afghanistan, Kandahar | Ausgabe von World Food Programme Hilfsgütern
Mamilioni ya watu nchini Afghanistan wanategemea misaada ya chakula kutoka mashirika ya hisani.Picha: Javed Tanveer/AFP/Getty Images

Vikwazo hivyo vya serikali ya Taliban vimesababisha ukosaaji mkubwa kwa ulimwengu. Utawala wa Taliban unasema unaheshimu haki za wanawake kwa tafsiri yao ya sheria ya Kiislamu na kwa sasa wanafanya kazi kutoa ufafanuzi wa muongozo wa kanuni za asasi za kiraia za wanawake. 

Lee pia alielezea uamuzi wa  Desemba wa mamlaka ya Taliban kupiga marufuku wanawake wa Afghanistan kufanya kazi katika asasi za kiraa kama jambo lingine baya.

Nikimnukuu hapa mkurugenzi huyo wa WFP kwa Afghanistan, anasema "Pamoja hali ilivyo sasa, mataifa washirika yanaendelea kufanya mapitio ya ufadhil nchini Afghanistan na upo uwezekano wa fedha kupungua zaidi."

Anasema wanufaika wengi wa msaada wa WFP ni wanawake na watoto. Pia alionesha hali ya kufanana kwa migogoro kwa mataifa kama Ukraine, pamoja na kadhia ya matetemeko ya ardhi ambayo yameyakumba matiafa ya Uturuki na Syria.

Lee amesema WFP inafuatilia kuhakikisha wanawake bado wako na uwezo wa kufikia maeneo ambayo ilisambaza pesa taslimu na chakula na hivyo mamlaka ilikuwa imetoa misamaha katika baadhi ya maeneo ili kuruhusu wanawake wahudumu katika asasi za kiraia.

Mamilioni ya Dola yanahitajika kuinusuru Afghanistan 

Afghanische Studentinnen / Online Unterricht
Wanawake nchini Afghanistan wanalazimika kujifunza wakiwa nyumbani baada ya utawala wa Taliban kupiga marufuku elimu ya sekondari na chuo kikuu.Picha: SAYED HASSIB/REUTERS

Shirika WFP limekuwa likifanya kazi sasa kuliko wafadhili wakubwa wa kawaida wa Afghanistan, kwa hivyo shirika hilo limetoa wito kwa mataifa ya kikanda na mashirika binafsi kuchangia kiasi cha dola milioni 800, kiwango ambacho kinaweza kusaidia umma katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Kwa mujibu wa rekodi za fedha za Umoja wa Mataifa, WFP ilipokea karibu dola bilioni 1.7 bilioni kwa mwaka uliopita kwa ajili ya Afghanistan.

Fedha hizo ni kutoka kwa serikali kadhaa na taasisi. Wafadhili wake wakuu ni pamoja na Marekani, Uingereza na Ujerumani.

Hata hivyo rekodi hazioneshi wahisani gani ambao wamepunguza mchango wao kwa mwaka huu.