UN: Afganistan inakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa
25 Oktoba 2021Katika ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa hii leo, Mkuu wa shirika la chakula duniani WFP David Beasley, amesema msimu huu wa baridi raia wa Afghanistan watalazimika kuchagua aidha kuihama nchi au kufa kwa njaa kama msaada wa dharura hautawafikia Waafghanistan kwa haraka.
Beasley, amesema Janga la Afghanistan ni kubwa zaidi kuliko hali ilivyo katika mataifa yanayokabiliwa na vita kama Yemen na Syria na pia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Afghanistan kwa sasa imeingia katika orodha ya mataifa yanayokabiliwa na mzozo mbaya kabisa wa kibinaadamu.
soma zaidi:Umoja wa Ulaya watoa yuro Bilioni moja kuisaidia Afghanistan
Kulingana na taarifa ya pamoja ya shirika la chakula duniani WFP na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, mmoja kati ya Waafghani wawili wanakabiliwa na mzozo wa chakula ulio katika kiwango cha tatu cha njaa na cha nne ambacho ni kiwango cha dharura.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema ni muhimu kuchukua hatua za haraka ili kuharakisha msaada kufika Afghanistan kabla ya msimu wa baridi ili kuepusha athari ya njaa na baridi itakayowakuta mamilioni ya watu wakiwemo wakulima, wanawake, watoto na wazee.
Taliban bado inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa
Mwezi Agosti kundi la Taliban liliipindua serikali iliyoungwa mkono na Marekani, kutangaza serikali ya mpito na kuapa kurejesha uthabiti nchini humo.
Lakini kundi hilo bado linakabiliwa na vikwazo vya kimataifa na kampeni ya mashambulizi mabaya dhidi yao kutoka kwa kundi hasimu linalojiita dola la kiislamu huku mabadiliko ya tabia nchi nayo yakichangia ukame wa mara kwa mara.
soma zaidi:Taliban yaahidi ulinzi zaidi misikiti ya Washia
Upande wa Magharibi mwa Afghanistan maelfu ya familia masikini tayari zimeuza mifugo na kutoroka makaazi yao na kutafuta makaazi mapya, chakula na usaidizi kutoka kwa makambi ya muda yalioko katika miji mikubwa.
Ziara iliyofanywa na muandishi habari wa shirika la AFP katika mikoa ya Herat na Badghis ilishuhudia baadhi ya familia zikilazimika kuwaozesha watoto wao wadogo wa kike ili kulipa madeni na kupata pesa za kununua chakula.
Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid hapo jana alisema wanajaribu kuwaondoa Waafghanistan katika hali wanayopitia kwa sasa huku akisema tayari misaada ya kibinaadamu imeanza kuwasili. Amesema kwa sasa wanapanga namna ya kusambaza chakula pamoja na nguo na hali itadhibitiwa hivi karibuni.
Chanzo: afp/ap