Waziri Mkuu wa Italia afanya ziara ya kushtukiza kwa Trump
5 Januari 2025Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloniamefanya ziara ya kushtukia na isiyo rasmi kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump katika makazi yake mjini Florida, taarifa hiyo ni kwa mujibu wa ofisi yake iliyotolewa leo Jumapili.
Picha mbalimbali zilizotolewa na ofisi ya waziri huyo mkuu wa mrengo wa kulia zimemuonesha akiwa kwenye mazungumzo na rais huyo mteule katika chumba cha mapokezi kwenye makazi ya Trump.
Soma zaidi.Meloni: Mashambulizi dhidi ya vikosi vya UNIFIL hayakubaliki
Giorgia Meloni anaungana na viongozi kadhaa wa kigeni, akiwemo Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambao wamemtembelea Trump, ambaye anatazamiwa kuapishwa kwa mara ya pili kuiongoza Marekani mnamo Januari 20.
Ziara ya Meloni imekuja muda mfupi kabla ya ziara ya siku nne ya Rais wa Marekani Joe Biden huko Roma, ambapo anatarajiwa kukutana naye pamoja na kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis kwa nyakati tofauti.