1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza: Watu 18 wauawa kwenye kambi ya UNRWA

12 Septemba 2024

Mamlaka ya Palestina imesema hivi leo kuwa takriban watu 18 wameuawa katika shambulizi la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4kXcT
Mfanyakati wa UNRWA akishuhudia uharibifu kwenye kambi ya Nuseirat
Mfanyakati wa UNRWA akishuhudia uharibifu kwenye kambi ya NuseiratPicha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

 Mashambulizi hayo ya jana usiku yaliendeshwa katika kituo kinachosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, ambapo raia wa Gaza walikuwa wametafuta hifadhi. Shule ya Al-Jawni huko Nuseirat ambayo mara kadhaa imekuwa ikishambuliwa kwa mabomu katika kipindi cha miezi 11 ya vita huko Gaza, iliachwa katika hali mbaya huku baada ya mashambulizi hayo.

Msemaji wa mamlaka ya ulinzi wa  raia wa Gaza  Mahmud Bassal amesema hii ni mara ya tano vikosi vya Israel vikishambulia kwa bomu shule hiyo ambayo imekuwa ikiwahifadhi watu 12,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu 18 wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, watoto na wanawake, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: BEN MCKAY/AAP/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya shule iliyogeuzwa kuwa makazi ya raia huko Gaza yaliwaua wafanyakazi wake sita wa shirika laUNRWA. Aidha Guterres ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X kuwa kinachotokea Gaza hakikubaliki kabisa.

Soma pia: Borrell: Vita vya Gaza ni "janga"

Hani Haniyeh, ni Mpalestina aliyelazimika kuyahama makazi yake na aliyekuwa akiishi katika kambi hiyo ya Nuseirat:

"Mlio wa mripuko ulilitikisa jengo. Tulitoka mbio na kushuhudia vipande vya miili vikiwa vimetawanyika kila mahali kwenye makazi haya. Bahati mbaya watoto wangu bado hawajulikani walipo. Wanangu wanne sijui walipo. Sijui wako wapi, hata mke wangu hulala hapa kwenye kona hii, lakini sijui yupo wapi."

Israel yajitetea kuwa ilikuwa ikiwalenga wanamgambo wa Hamas

Gaza I Mamlaka ya Palestina wamesema kambi hiyo huwahifadhi raia
Mamlaka ya Palestina wamesema kambi hiyo huwahifadhi raia, wengi wao wakiwa wanawake na watotoPicha: Moez Salhi/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo, jeshi la Israel limesema liliendesha shambulizi lenye usahihi dhidi ya kituo cha Hamas na kwamba hatua kadhaa zilichukuliwa ili kuepusha hatari kwa raia. Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Israel vimeshambulia shule kadhaa huko Gaza wakidai kuwalenga wanamgambo wa Hamas wanaoendesha shughuli zao maeneo hayo na kujificha miongoni mwa raia, madai ambayo kila mara yamekuwa yakikanushwa na Hamas.

Soma pia: Watu 40 wauawa katika kambi ya al-Mawasi huko Gaza

Umoja wa Mataifa umekumbushia kuwa shule na miundombinu mingine ya kiraia haitakiwi kulengwa na mashambulizi na ni lazima ilindwe wakati wote. Mara kwa mara Gaza imekuwa ikitajwa kuwa mahali hatari zaidi duniani kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu. Mkuu wa  UNRWA Philippe Lazzarini amesema baada ya shambulizi hilo kwamba wafanyakazi wasiopungua 220 wa shirika hilo wameuawa katika vita hivi vya Gaza vilivyoanza Oktoba 7 mwaka jana. Kulingana na Wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, hadi sasa Wapalestina 41,118 wameuawa.

(DPAE,AP,AFP)