1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Watu 40 wauawa katika kambi ya al-Mawasi, Gaza

10 Septemba 2024

Takriban watu 40 wameuawa na wengine 60 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya al-Mawasi katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4kSRN
Shambulizi la Israel katika kambi ya al-Mawasi huko Gaza
Shambulizi la Israel katika kambi ya al-Mawasi huko GazaPicha: Jehad Alshrafi/Anadolu/picture alliance

Shirika la habari la Palestina WAFA limeripoti kuwa Israel ilishambulia vikali mapema leo Jumanne  katika eneo wanakoishi wakimbizi wa ndani. Lilikuwa shambulio kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kambi ya  al-Mawasi yenye msongamano wa watu wanaoishi kwenye mahema huko Gaza, eneo ambalo Israel ililiteua kuwa la kibinadamu kwa mamia ya maelfu ya raia wanaotafuta eneo salama ili kuepuka vita hivyo. 

Shambulizi la leo liliacha mashimo yenye urefu wa hadi mita 10 huku watu 40 wakiuawa na wengine zaidi ya 60 wakiwa wamejeruhiwa. Kikosi cha Ulinzi wa Raia cha Gaza kimesema kuwa maafisa wake wa kwanza kuwasili eneo hilo walipata miili 40 na walikuwa bado wanaendelea kuwatafuta watu wengine na kusisitiza kuwa wapo watu wa familia moja waliouawa kufuatia mashambulizi hayo. Raed Muammar, binti yake aliuawa katika shambulio hilo:

Makumi ya Wapalestina wameuawa kufuatia shambulio huko Al-Mawasi,Gaza
Makumi ya Wapalestina wameuawa kufuatia shambulio huko Al-Mawasi,GazaPicha: Abdallah F.s. Alattar/Anadolu/picture alliance

" Mida ya saa saba na nusu usiku, tulikuwa tumelala wakati yalipoanza mashambulizi makali ya Israel. Binti yangu ameuawa kama shahidi; mke wangu na binti yangu mwingine wamejeruhiwa na mahali hapa pameharibiwa kabisa. Kuna mabaki ya mahema tu. Tulikuwa katika maeneo yaliyoteuliwa kuwa ya kibinadamu ambayo yalipaswa kuwa salama nayo ni al-Mawasi hapa Khan Younis. Watoto hawa ndio Israel inaowalenga, hebu tazama mwenyewe."

Soma pia: Hamas na Israel zinapaswa kuafikiana kusitisha vita Gaza

Jeshi la Israel limesema lilikuwa linawalenga wanamgambo wa Hamas waliokuwa wakiendesha shughuli zao eneo hilo na kwamba walitumia silaha zenye usahihi na njia nyinginezo ili kuepusha vifo vya raia.

Lakini kundi la Hamas limetoa taarifa ya kukanusha uwepo wa wapiganaji katika eneo hilo. Hata hivyo Israel na Hamas hawakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yao.

Hali ya kiafya ni tete huko Gaza

Mkuu wa shirika la UNRWA  Philippe Lazzarini
Mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini Picha: Salvatore Di Nolfi/Keystone/dpa/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa ndani wa Kipalestina  UNRWA  limesema kuwa jeshi la Israel lilizuia hapo jana msafara wake kwa zaidi ya saa nane licha ya mpango huo kuratibiwa na jeshi la nchi hiyo. Mkuu wa shirika hilo Philippe Lazzarini amesema wafanyakazi waliozuiliwa walikuwa wakijaribu kushiriki katika kampeni ya chanjo ya polio huko Gaza.

Kampeni hiyo ilizinduliwa baada ya madaktari kugundua ya  maambukizi ya kwanza katika kipindi cha miaka 25. Kampeni hiyo inalenga kutoa chanjo ya Polio kwa watoto 640,000 wa Gaza katika wakati ambapo vita hivi vilivyoanza Oktoba 7 mwaka jana vimeharibu pakubwa mifumo ya huduma za afya. Madaktari na wataalam wa masuala ya afya wanasema ugonjwa unaweza kuwa 'hukumu ya kifo' huko Gaza kwani vita vinachochea maradhi na wagonjwa hawapati matibabu wanayostahili.

(Vyanzo: APE, Reuters)