Watu 11 wauawa katika mji alikozaliwa Volodymir Zelensky
13 Juni 2023Mamlaka ya mji wa Kryvyi Rih imesema idadi ya watu waliofariki kutokana na mashambulio hayo ya Urusi inaweza kuongezeka. Taarifa zaidi zinafahamisha kuwa watu 28 wamejeruhiwa pale makombora ya Urusi yalipopiga jengo la ghorofa tano ambalo liliteketea moto.
Gavana Serhiy Lysak wa mkoa wa Dnipropetrovsk amesema uharibifu huo katika mji aliozaliwa Rais Volodymyr Zelenskyy ni hatua ya umwagaji damu ya hivi karibuni katika vita vya Urusi nchini Ukraine, vilivyoanza mwezi Februari mwaka 2022, wakati ambapo vikosi vya Ukraine vikiendelea na operesheni za kuwafurusha Warusi kwa kutumia zana zilizotolewa na nchi za Magharibi.
Soma:Ukraine yaanza mashambulizi kuyakomboa maeneo yake
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema jeshi lake limeshambulia kwa makombora bohari la kuhifadhia risasi na zana nyingine za kivita zinazotoka katika nchi za Magharibi katika mji wa Kharkiv, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine. Gavana wa eneo hilo Oleh Syniehubov amefahamisha kwamba watu wawili wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo katika mji wa Shevchenkove, kusini mashariki mwa Kharkiv.
Wakati huo huo Ufaransa leo imefichua kampeni kubwa ya upotoshaji ya Urusi, huku habari za uwongo zenye kuonesha chuki dhidi ya Ukraine zikionekana kana kwamba zilichapishwa na vyombo vya habari maarufu vya nchini Ufaransa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna amesema vitendo hivi havistahili kufanywa na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kwingineko mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nishati ya atomiki IAEA, Rafael Grossi ameutembelea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv kukutana na Rais Volodymyr Zelenskiy na pia anapanga kukitembelea kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachokaliwa na Urusi baada ya mto mkubwa karibu na hapo kuharibiwa wiki iliyopita.
Soma:Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anapanga kuzungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin
Naye Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO Jens Stoltenberg amesema leo kabla ya mkutano wake na Rais wa Marekani Joe Biden kwamba mashambulizi ya Ukraine ya kuyakomboa maeneo mengi yanayokaliwa kwa mabavu na Urusi yanaweza kuilazimisha Urusi kukubali kufanya mazungumzo.
Vyanzo:DPA/AFP/RTRE