Ukraine yaanza mashambulizi kuyakomboa maeneo yake
12 Juni 2023Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wanajeshi wa Ukraine wakisherehekea katika makazi jirani ya Blahodatne na Neskuchne katika jimbo la Donetsk. Naibu waziri wa ulinzi wa Kyiv alisema eneo la Makarivka nalo litakombolewa hivi karibuni.
Mafanikio makubwa ya kijeshi ya Ukraine katika eneo la Zaporizhzhia yatawezesha vikosi vyake kushikilia daraja linalounganisha Urusi na eneo la Crimea, ambayo itakuwa ni pigo kubwa kwa Urusi. Moscow bado haijathibitisha kuanguka kwa kijiji chochote, badala yake inazungumza juu ya kuzima mashambulizi ya Ukraine katika eneo hilo.
Waendesha mshtaka wa jimbo la Kherson wamesema watu watatu waliuawa na wengine 23 kujeruhiwa Jumapili wakati Urusi iliposhambulia kwa makombora boti ya uokoaji ikiwaondoa raia kutoka eneo linalodhibitiwa na Urusi. Msemaji wa jeshi la Ukraine Valeriy Shershen amesema wamewashika wanajeshi kadhaa wa Urusi na wapiganaji wanaowaunga mkono kufuatia mapigano ya hapo jana Jumapili.
Mashambulizi ya makombora
Rais Volodymyr Zelensky alithibitisha kwamba mashambulizi ya kukabiliana na Urusi yameanza, huku akiituhumu Urusi kuwashambulia raia wa Ukraine.
''Magaidi wa Urusi wanaendelea kushambulia kwa makombora njia za uokoaji, sehemu za uokoaji, na boti ambazo watu wanaokolewa. Leo, kutokana na moja ya makombora haya, watu 3 wameuawa, rambirambi zangu kwa jamaa na marafiki. Watu wengine walijeruhiwa, ikiwa ni pamoja na polisi wawili.'',alisema Zelensky.
Kwingineko, Ukraine inasema Urusi imelipua bwawa jingine katika eneo la Zaporizhzhia, kufuatia uharibifu wa jengo kuu la Nova Kakhovka siku ya Jumatatu, ambalo lilisababisha mafuriko makubwa.
Maafisa wa Ukraine wanasema watu saba walifariki na watu 35 wakiwemo watoto saba bado hawajulikani walipo kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokana na uharibifu wa bwawa hilo. Ukraine na Urusi zinatupiana lawama katika uharibifu wa bwawa hilo.
Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa
Huku hayo yakijiri, Ukraine na Urusi walibadilishana wafungwa wa kivita. Mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, Andriy Yermak amesema kuwa Kyiv iliwarejesha wanajeshi 95 ambao walikamatwa na Warusi katika vita vya miji ya Bakhmut na Mariupol na kwa upande wake Urusi iliwapokea wanajeshi wake 90 katika ubadilishaji mpya wa wafungwa.
Katika juhudi za kuisaidia Ukraine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana leo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na kiongozi wa Poland Andrzej Duda mjini Paris, Ufaransa kabla ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami ya NATO mwezi ujao.
Chanzo: AFP