1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi wamepiga kura kumchagua rais.

20 Mei 2020

Raia wa Burundi leo wanapiga kura katika uchaguzi muhimu wa urais, bunge na madiwani. Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema kwa ujumla zoezi hilo limeendeshwa katika mazingira ya utulivu.

https://p.dw.com/p/3cXwG
Coronavirus - Präsidentschaftswahl in Burundi
Picha: picture-alliance/dpa/B. Mugiraneza


Hata hivyo, wananchi wengi wamekosoa hatua ya kufungwa kwa mitandao ya kijamii wakati kura zilipoanza kupigwa.  Katika vituo mbali mbali vya kupigia kura vya mjini Bujumbura kumeshuhudiwa raia wakipiga kura kuanzia 12 asubuhi kama ilivyopangwa na tume CENI, huku vikosi vya  jeshi na polisi vikipiga doria kuhakikisha usalama.

Baadhi ya raia waliozungumza na DW wameonesha matumani ya kuimarika kwa usalama wa tafa hilo baada ya kupatikana kwa kiongozi mpya miongoni mwa wagombea. Na mwininge alitahadharisha ili kuepukana na ghasia za baada ya uchaguzi kuna umuhimu wa kuwepo na uwazi. Huku mwingine akikosoa kuona kwenye siku hii ya uchaguzi mawasiliano ya intaneti kwenye mitandao ya kijami yakiwa yamesitishwa.

Raia wa Burundi waonesha matumaini mapya.

Coronavirus - Präsidentschaftswahl in Burundi
Baadhi ya raia wa Burundi wakipiga kuraPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Kurejeshwa kwa uhusiano wa kimataifa ni suala jingine ambalo linapewa kipaumbele na wapigakura nchini hapa, baada ya miaka kadhaa ya Burundi kutengwa chini ya utawala wa Rais Pierre Nkurunziza. Msemaji wa Polisi ya taifa Pierre Nkurikiye amebainisha hivi punde tu kwamba kuna wafuasi kadhaa wa chama cha upinzani CNL cha Agathon Rwasa waliokamatwa katika tarafa ya Kanyosha  Bujumbura vijijini, Muramvya na Rumonge  wakituhumiwa kutaka kuvuruga usalama.

Naye Rwasa aliyepigia kura katika mkoa wake wa kuzaliwa wa Ngozi amesikika akikosoa kubugudhiwa waangalizi wa chama chake katika mikoa Rumonge na Bujumbura Vijijini.Balozi wa Tanzania nchini Burundi Jilly Maleko Maleko amekaribisha uchaguzi
huu huku akizitaka pande tafauti kukubaliana na matokeo.

Rais Nkurunziza baada ya kupiga kura amekumbusha umuhimu wa uchaguzi huu uliogharamiwa na raia. Matokeo ya uchaguzi huu yatatangazwa ijumaa wiki hii.