1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warundi wanamchagua rais mpya

Admin.WagnerD20 Mei 2020

Raia wa Burundi wanapiga kura leo ya kumchagua rais mpya, wabunge na madiwani, licha ya janga hili la Corona. Wagombea wakuu ni Jenerali Evariste Ndayishimiye wa CNDD-FDD na mpinzani Agathon Rwasa wa CNL.

https://p.dw.com/p/3cW40
Bildkombo Agathon Rwasa und Evariste Ndayishimiye
Picha: DW/A. Niyirora

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tokea saa 12 asubuhi saa za afrika ya kati, kuchagua mmoja kati ya wagombea saba wanaowania kuchukua nafasi ya rais Pierre Nkurunziza atakayeondoka baada ya kuongoza kwa miaka 15. 

Miongoni mwa wagombea wakuu kwenye uchaguzi huo ni pamoja na jenerali Evariste Ndayishimiye kutoka chama tawala cha CNDD-FDD na Agathon Rwasa ,kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CNL. Kwenye baadhi ya majimbo vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kama kawaida, kwenye shule ya msingi ya Bugera,mkoani Ndava kwenye jimbo la Mwaro katikati mwa nchi ,kiongozi wa kituo hicho cha uchaguzi, Prosper Sindayihebura alisema kwamba walipokea vifaa vyote vya uchaguzi toka jana na shughuli za uchaguzi zinaendelea vizuri.

Jiji la Bujumbura limekuwa na misururu mirefu ya wapiga kura.

Burundi | Coronavirus
Raia wa Burundi miongoni mwao na barakoaPicha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Mjini Bujumbura,mji mkuu wa Burundi, misusuru mirefu ya wapigaji kura ilishuhudia tangu saa 11 asubuhi,yaani saa moja kabla ya kufunguliwa vituo vya uchaguzi. Aidha wakazi wa Bujumbura wameshuhudia kukatwa kwa intaneti na mitandao ya kijamii muda mchache tu kabla ya kufunguliwa kwa vituo vya uchaguzi.

Burundi ilikataa kuweka sheria kali dhidi ya ugonjwa wa COVID-19,huku ikiwashauri raia wake wapatao milioni 11,kuzingatia kanuni za usafi na kuepuka mikusanyiko pale inapowezekana. Lakini mikutano ya kampeni za kisiasa ilishuhudiwa kukusanya watu wengi ambao hawakuzingatia kanuni hizo za kiafya. Hadi sasa serikali ya nchi hiyo imerekodi visa 42 vya maambukizi ya virusivya corona na kifo kimoja kutokana na janga hilo.

Burundi | Coronavirus
Wafuwasi wa chama tawala nchini Burundi Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/B. Mugiraneza

Kampeni zilivurugwa na ghasia baada ya wapinzani kulalamika kunyanyaswa na polisi.

Kampeni  za uchauguzi huo zilighubikwa na ghasia na upinzani kulalamika kwamba wafuasi wake kadhaa walikamatwa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Kampeni hiyo ilionyesha ushindani mkuu baina ya mgombea wa chama tawala Evariste Ndayishimiye na Agathon Rwasa wa chama kikuu cha upinzani cha CNL.

Evariste Ndayishimiye,mwenye umri wa miaka 52, ameungwa mkono na rais Nkurunziza. Ni katibu mkuu wa chama cha CNDD-FDD, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na alikuwa kamanda muasi, pamoja na Nkurunziza wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyomalizika 2003.Na Agathon Rwasa,mwenye umri wa miaka 56 ni kutoka kundi la zamani la uasi la Palipehutu-FNL,moja wapo ya makundi makubwa mawili ya waasi mnamo miaka ya tisini.

Tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1962, Burundi imeshuhudia wimbi baada ya wimbi la ghasia za kisiasa na kikabila, lakini raia wake wanamatumaini ya mwanzo mpya.

Mashirika AFPE/APE/AFPF