Israel yataka kuubadilisha mpango wa kusitisha vita Gaza
26 Julai 2024Hatua hii inatatiza mchakato wa kufikiwa makubaliano ya mwisho ya kusitisha mapigano yanayoendelea kwa miezi tisa sasa na kusababisha uharibifu mkubwa kwenye eneo hilo.
Duru kutoka magharibi pamoja na Misri zimearifu leo kuhusiana na nia hiyo ya Israel ya kutaka kubadilisha mkondo kwenye mpango huo.
Israel inasema Wapalestina waliokimbia makazi yao wanatakiwa kuhakikiwa wakati wanarejea kaskazini mwa Gaza wakati makubaliano yatakapoanza kutekelezwa, kinyume na yale ya awali yaliyosema wanaweza kurudi nyumbani bila ya masharti yoyote, vyanzo vinne vimeiambia Reuters. Wakazi hao waliyakimbia mapigano yaliposhika kasi huko kaskazini, na kwenda eneo la kusini, kujihifadhi.
Soma pia:UN yaelezea hofu kuhusu mapigano yanayoendelea Khan Younis
Afisa mmoja wa magharibi amesema wapatanishi wa Israel wanataka mfumo wa ukaguzi kutokana na hofu pengine wakazi wanaorejea wanaweza kuwasaidia wapiganaji wa Hamas waliosalia Gaza.
Lakini, Hamas hawataki hata kusikia masharti haya mapya, vimesema vyanzo vya Palestina na Misri. Lakini afisa mmoja mwandamizi wa Israel alisema Hamas bado hawajayaona mapendekezo haya mapya yatakayotolewa hivi karibuni.
Je, Netanyahu atazungumza nini na Trump?
Na kutoka Washington, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakaribia kukutana na mgombea urais kupitia chama cha Republican Donald Trump huko Florida, katika mazungumzo ambayo huenda yakalegeza mivutano kati ya viongozi hao waliowahi kuwa maswahiba, wakati Trump akiwa rais wa Marekani.
Mkutano wao unafanyika siku moja baada ya Netanyahu kukutana na Rais Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris mjini Washington. Netanyahu, alilazimika kubadilisha mpangilio wa ziara yake, ili aweze kukutana na Trump.
Lakini kutoka huko Jerusalem, maafisa wa ngazi za juu wamenukuliwa wakimkosoa Harris anayetarajiwa kugombea urais kupitia chama cha Democratic, aliyemwambia Netanyahu katika mkutano wao kwamba huu ni muda wa kuvimaliza vita vya Gaza.
Mawaziri wa Fedha Bezalel Smotrich na Usalama wa Taifa Ben-Gvir, wanaoongoza vyama viwili vya kidini vyenye misimamo mikali na ushawishi kwenye serikali ya muungano ya Netanyahu, wamelaani matamshi ya Harris. Ben-Gvir aliandika kwenye ukurasa wa X "Ndugu mgombea, uhasama hautakoma."
Australia yasisitiza kusitishwa vita huko Gaza
Na huko Laos, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong ametoa wito katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN wa kusitishwa mapigano huko Gaza na kuhitimishwa kile alichokiita mateso dhidi ya Wapalestina ambayo hayakubaliki.
"Kwa bahati mbaya, janga la kibinaadamu linajitokeza Gaza. Mateso kwa raia hayakubaliki na Australia inaamini watu wa Palestina hawatakiwi kulipa gharama ya kuangushwa Hamas. Makubaliano ya kusitishwa mapigano ni lazima yafikiwe."
Tukimalizia na huko Geneva, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki katika ardhi za Palestina Francesca Albanese amekabiliwa na ukosoaji mkali kutoka Israel, baada ya kuweka chapisho mtandaoni akimfananisha Netanyahu na Adolf Hitler.
Soma pia: Netanyahu atetea vita vya Gaza wakati akilihutubia bunge la Marekani
Albanese, mwezi Machi pia alikosolewa na Israel baada ya kuishutumu kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza. Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel iliandika kupitia mtandao wa X ikisema "Haiwezekani Albanese aendelee kutumia Umoja wa Mataifa kama ngao ya kueneza chuki dhidi ya Wayahudi."