1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN yaelezea hofu kuhusu mapigano yanayoendelea Khan Younis

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2024

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea wasiwasi juu ya mapigano yanayoendelea katika mji wa Khan Younis yaliyowalazimu watu zaidi kukimbilia katika mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Gaza.

https://p.dw.com/p/4byqd
Wanajeshi wa Israel karibu na jengo lililoharibiwa wakati wa oparesheni mjini Khan Younis
Wanajeshi wa Israel karibu na jengo lililoharibiwa wakati wa oparesheni mjini Khan YounisPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Msemaji katika ofisi hiyo Jens Laerke amesema mapigano hayo yamesababisha ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi wa ndani wanaotafuta hifadhi mjini Rafah katika siku za hivi karibuni.

Aidha, ofisi hiyo imeutaja mji huo kuwa eneo lisilokalika na kwamba watu wamekata tamaa.

Kauli hiyo imetolewa wakati Israel ikijiandaa kusonga mbele katika vita vyake kuelekea zaidi upande wa kusini mwa Gaza, karibu na mpaka na Misri.

Zaidi ya nusu ya wakaazi milioni 2.3 wa Gaza wamejihifadhi katika eneo hilo, wakikabiliwa na baridi kali na njaa katika mahema ya muda na majengo ya umma.