Wafuasi 40 wa Bobi wakamatwa Uganda kwa kuandamana
11 Machi 2021Siku ya Jumanne, kiongozi wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi al maarufu Bobi Wine aliwahimiza wafuasi wake kushiriki maandamano ya amani kupinga matokeo ya urais na pia dhidi ya kamatakamata ambayo Rais Yoweri Museveni amekariri inalenga kukabiliana na majaribio ya kusababisha ghasia.
Bobi Wine aliwahutubia baadhi ya wafuasi wake kwenye makao makuu ya chama hicho ambako alionyesha majalada kadhaa akisema ni fomu za matokeo ya uchaguzi alizokuwa amewasilisha mahakamani kama ushahidi.
Soma pia: Maoni: Ushindi wa Museveni ni wa mashaka
Vyombo vya usalama vimeitikia tangazo hilo la maandamano ya amani kwa kuweka doria kali sehemu mbalimbali za miji na wamethibitisha kuwakamata zaidi ya wafuasi 40 wa chama cha NUP waliokutwa wakishiriki maandamano.
Msemaji wa polisi wa Kampala, Patrick Onyango ameonya kuwa wataendelea na operesheni ya kuwakamata watu wanaoshiriki maandamano, akiwashauri wafuasi wa NUP kutoitikia wito wa kiongozi wao ambao unaweza kusababisha ghasia na uharibifu wa mali za watu.
Lakini msemaji wa NUP, Joel Senyonyi amesisitiza kuwa wataendelea na maandamano hayo ya amani huku wakiitaka serikali kuwaachia wafuasi wao zaidi ya 400 ambao wanashikiliwa na vyombo vya usalama bila kufikishwa mahakamani.
Utawala wakosolewa kwa utekaji wa watu
Shirika la kimataifa ya haki za binaadamu, Human Rights Watch limetoa taarifa za kuukosoa utawala wa Uganda kwa mienendo yake ya kuukandamiza upinzani pale inapowateka nyara wafuasi wao ikihimiza uchunguzi kuhusu hali hii kufanyika na kuwaachia huru watu waliokamatwa.
Soma pia: Museveni aongoza matokeo ya awali nchini Uganda
Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Museveni alithibitisha kuwa takriban watu hamsini wanazuiliwa na kikosi chake cha ulinzi, SFC kuhusiana na jaribio la kushiriki ghasia.
Wiki iliyopita Mahakama ya Juu ilimruhusu Bobi Wine kuondoa kesi ya malalamiko aliyokuwa amewasilisha akipinga hatua ya tume ya uchaguzi ya Uganda kumtangaza Rais Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika mwezi Januari.
Lakini tume ya uchaguzi imeyataja matokeo ambayo Bobi Wine amelezea kuwa yalimpa ushindi wa asilimia 54 kuwa ya kupotosha.
Bobi Wine alitamka kuwa chanzo cha kutangaza maandamano ni matokeo batili yaliyotolewa na tume hiyo. Askari wa vyombo vya usalama wameshuhudiwa wakiweka doria katika sehemu mbalimbali za mji wa Kampala. Yumkini hii ni katika hatua ya kukabiliana na majaribio yoyote ya maandamano.