1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Bobi Wine kufikishwa katika mahakama ya kijeshi

16 Oktoba 2020

Zaidi ya wafuasi 130 wa chama cha NUP kinachongozwa na mwanasiasa wa Uganda Robert Kyagulanyi watafikishwa katika mahakama ya jeshi kujibu mashtaka ya kupatikana na vitu vinavyodaiwa kuwa sare za kijeshi

https://p.dw.com/p/3k0zR
Uganda | Razzia Kampagnenzentrale Bobi Wine Anhänger
Picha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture-alliance

Hata hivyo, wanasiasa mbalimbali wamelezea kesi hiyo kuwa ya kisiasa inayolenga kuwatia hofu na mashaka wafuasi wa Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. 

Wafuasi hao  132 walikamatwa siku mbili zilizopita wakati polisi na majeshi walipovamia makao makuu ya chama hicho na kutwaa kofia aina ya bereti, mavazi mbalimbali na pia picha za mgombea urais mtarajiwa Robert Kyagulanyi al maarufu Bobi Wine. Wafuasi 50 walikamatwa kwenye makao makuu hayo, 38 kwenye mtaa wa Kamwokya na wengine walikamatwa katikati ya mji kwenye biashara zao wakishona mavazi mekundu.

Uganda Kampala Festnahme Bobi Wine
Ofisi za Bobi Wine zilivamiwa na nyaraka zake kuporwaPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Aidha inadaiwa watu hao wameanza kujenga tabia ya kijeshi kwa kubuni kile kinachodaiwa kuwa kikosi. Akizungumza kwa njia ya simu na DW, msemaji wa majeshi Brigedia Flavia Byekwaso amefafanua kuwa watu hao wanachukuliwa kujihusisha katika kuvunja sheria za kijeshi na ndiyo maana watafikishwa katika mahakama ya kijeshi

Msemaji wa polisi eneo la Kampala Patrick Onyango ameongezea kuwa vitendo vya vijana kuvalia nembo na mitindo ya kijeshi imezidi licha ya onyo kutolewa mara kadhaa. Hata hivyo viongozi mbalimbali wa kisiasa wametaja kamatakamata ya wafuasi wa Bobi Wine kuwa hila ya utawala kuwatia hofu wafuasi wake na kuendelea kutatiza mandalizi ya chama cha NUP. 

Wakati huohuo, mahakama imeahirisha maamuzi kuhusu kesi ya uhalali wa chama cha NUP ambayo yangetolewa leo. Maamuzi hayo yamesubiriwa kwa hamu na ghamu na wafuasi na wagombea wa chama hicho ili kubaini kama hatashiriki katika uchaguzi au la. Maamuzi hayo ndiyo yatamhakikishia Bobi Wine kama ataweza kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, vinginevyo huenda asiidhinishwe kugombea.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala