1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Waasi wa Yemen na serikali wamaliza kubadilishana wafungwa

16 Aprili 2023

Waasi wa Yemen na vikosi vya serikali wamewaachia mamia ya wafungwa katika siku ya mwisho ya utekelezaji wa makubaliano ya kubadilishana wafungwa karibu 900.

https://p.dw.com/p/4Q9KL
Baadhi ya wafungwa wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Sanaa wakati wa zoezi la kubadilishana wafungwa kati ya waasi na serikali huko Yemen.
Yemen imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu hatua iliyolitumbukiza taifa hilo katika mizozo kuanzia ya kiuchumi hadi kibinaadamu.Picha: KHALED ABDULLAH/REUTERS

Ndege zilizobeba wafungwa ziliondoka kwa wakati mmoja kutoka katika mji wa Sanaa, unaodhibitiwa na waasi wa Houthi na ule wa Marib ulioko chini ya serikali, hii ikiwa ni kulingana na Kamati ya Kimataifa ya msalaba Mwekundu, ICRC.

Ndege tatu nyingine zitakazoondoka mchana huu ndizo zitakazobeba kundi la mwisho la wafungwa hao wa kivita na kuhitimisha makubaliano yaliyofikiwa Uswisi mwezi uliopita ya kubadilishana wafungwa 181 wa serikali na waasi 706.

Kiongozi wa kisiasa wa upande wa waasi Mahdi al-Mashat amesema awamu inayofuata ya mazungumzo na Saudi Arabia, inayoongoza muungano wa kijeshi dhidi ya Wahuthi huenda ikaanza baada ya sikuku za Eid al-Fitr zinazotarajiwa kufanyika tarehe 21, shirika la habari la Yemen la Saba, limeripoti.