1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji kadhaa wauwawa Kenya

25 Juni 2024

Watu kadhaa wameuwawa kwa kupigwa risasi karibu na maeneo ya bunge nchini Kenya, wakati waandamanaji walio na hasira walipovunja vizuizi na kuingia maeneo hayo. zaidi ya watu wengine 50 wamejeruhiwa katika vurugu hizo.

https://p.dw.com/p/4hTwW
Kenia Proteste gegen geplante Steuererhöhungen in Nairobi
Picha: James Wakibia/ZUMA Press Wire/IMAGO

Sehemu ya maeneo ya bunge nchini Kenya yamechomwa moto wakati maelfu ya waandamanaji wanaopinga mswada tete wa fedha, walipovamia katika maeneo hayo.

Wabunge waliokuwa ndani ya bunge, inasemekana walitoroshwa na kupelekwa sehemu salama. Hatua hiyo ya waandamanaji kuvamia maeneo ya bunge ni shambulizi la moja kwa moja kwa serikali ambalo halijawahi kuonekana kwa miongo kadhaa. 

Polisi wa Kenya wafyatua mabomu ya machozi kwa waandamanaji

Moja ya matakwa ya waandamanaji ni wabunge hao kutoupigia kura mswada huo wa fedha, unaotaka kuwatoza wananchi ushuru zaidi katika nchi hiyo ambayo tayari watu wake wanapambana na kupanda kwa gharama ya maisha.

Waandamanaji wakasirishwa na hatua ya wabunge kupitisha mswada wanaoupinga

Kenia | Proteste gegen geplante Steuererhöhungen in Nairobi
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Waandamanaji waliwashinda nguvu polisi na kuingia bungeni muda mfupi baada ya wabunge kupitisha muswada huo, ambao sasa  unasubiri saini ya Rais William Ruto kuwa sheria kamili. Waandamanaji hao hata hivyo waliwaruhusu wabunge wa upinzani walioupinga mswada huo kuondoka katika maeneo hayo  waliyoyazingira.

Kijana wa pili athibitishwa kufa katika maandamano ya Kenya

Ofisi ya gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye pia ni mwanachama wa chama tawala, imechomwa. Ofisi hiyo ipo karibu na maeneo ya bunge. Polisi kwa sasa wanatumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuendelea kuwatawanya waandamanaji waliojawa na hasira, waliosikika wakisema watawaandama wanasiasa wote.  

Tume ya haki za binadamu ya Kenya KHRC, imesema katika taarifa iliyoitoa kupitia ukurasa wa X kuwa "polisi wamewapiga risasi waandamanaji wanne na kumuua mmoja, tunalaani vikali mauaji ya polisi".

Mmoja auwawa, 200 wajeruhiwa katika maandamano ya Kenya

afp/ap