1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Vita vya Israel-Hamas vyazusha hofu ya ugaidi katika EU

5 Desemba 2023

Kamishna wa Masuala ya Ndani katika Umoja wa Ulaya ametoa tahadhari kwamba umoja wake unakabiliwa na kitisho kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/4ZoTE
Israel yatanua mashambulizi yake Gaza
Israel yatanua mashambulizi yake GazaPicha: Ahmed Zakot/SOPA Images via ZUMA/dpa/picture alliance

Tahadhari ya kamishna wa Masuala ya Ndani ya Umoja wa Ulaya Ylva Johansson, kuhusu kitisho kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi katika umoja huo, inajiri mnamo wakati uchunguzi unaendelea dhidi ya shambulizi la mwisho wa wiki mjini Paris Ufaransa.

Maswali yaliibuka kuhusu afya ya akili ya mshukiwa wa shambulizi hilo, ambaye kabla ya kumchoma kisu na kumuua mtalii wa Kijerumani na kuwajeruhi wengine wawili, alikula kiapo cha utii kwa kundi lenye misimamo mikali ya dini linalojiita pia Dola la Kiislamu.

Akizungumza na waandishi Habari mjini Brussels alipowasili kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa masuala ya ndani wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Kamishna Ylva Johansson alisema pamoja na vita kati ya Israel na Hamas na mgawanyiko ambao vita hivyo vinasababisha katika jamii, na wakati msimu wa sikukuu ukikaribia, kuna hatari kubwa ya kufanyika mashambulizi ya kigaidi katika Umoja wa Ulaya.

"Tuliona hivi karibuni mjini Paris, kwa bahati mbaya tumeyaona pia hapo nyuma, kwa hivyo huu ni mjadala muhimu tutakaokuwa nao leo kwenye mkutano wetu. Nitatangaza pia kuwa tutatenga euro milioni 30 zaidi kwa ajili ya ulinzi, kwa mfano katika hali hii, kwenye maeneo ya kuabudu,” amesema Johansson.

Kamishna wa Mambo ya Ndani katika Umoja wa Ulaya Ylva Johansson
Kamishna wa Mambo ya Ndani katika Umoja wa Ulaya Ylva JohanssonPicha: MENELAOS MYRILLAS/SOOC/AFP/Getty Images

 Israel yatanua vita Gaza Kusini hofu ikitawala kuhusu vifo vya raia

Waandamanaji wajitokeza katika miji ya Ulaya

Katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono Wapalestina, wanaounga mkono Israel na vilevile wanaopinga chuki dhidi ya Wayahudi, wamekuwa wakijitokeza katika miji kadhaa mikuu ya Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser ameeleza kuwa shambulizi la Paris, linaonyesha jinsi tishio la ugaidi unaofanywa na makundi yenye misimamo mikali ya Kiislamu ni kubwa katika Umoja wa Ulaya, na vita vya Gaza vinazidisha hali hiyo.

Haya yanajiri mnamo wakati Israel imeanza mashambulizi karibu na mji wa pili kwa ukubwa katika Ukanda wa Gaza Khan Younis.

Hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi'

Aidha roketi iliyofyatuliwa kutoka Gaza imepiga nyumba moja katika pwani ya Israel Ashkelon. Polisi ya Israel imesema hayo Jumanne.

Waandamanaji wanaowaunga mkono Wapalestina wakijitokeza kwenye mitaa ya London Novemba 11, 2023.
Waandamanaji wanaowaunga mkono Wapalestina wakijitokeza kwenye mitaa ya London Novemba 11, 2023.Picha: Henry Nicholls/AFP/Getty Images

Amiri wa Qatar aikosoa Israel

Kwingineko, Amiri wa Qatar Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani, amewalaani baadhi ya viongozi wa kimataifa kwa kutounga mkono usitishaji vita Gaza. Amesema hayo alipouhutubia mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa ya Ghuba mjini Doha Qatar.

Mkutano huo wa ushirikiano wa kimaendeleo unafanyika wakati mapigano kati ya Israel na Hamas yameanza tena.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pia alihudhuria mkutano huo wa Doha na amedai kwamba mauaji ya Wapalestina ni uhalifu wa kivita na dhidi ya ubinadamu.

Israel inasema imepania kusambaratisha miundo mbinu ya kijeshji ya Hamas na kuliondoa kundi hilo madarakani ili kuzuia shambulizi jingine dhidi yake kama la Oktoba 7, ambalo lilichochea vita.

Vita vya Israel-Hamas: IDF yatanua mashambulizi ya ardhini Gaza

Shambulizi hilo la kushtukiza kusini mwa Israel lilisababisha vifo vya watu 1,200, wengi wakiwa raia. Aidha wanamgambo wa Hamas waliwachukuwa mateka takriban watu 240 wakiwemo watoto na wanawake.

Marekani | Waandamani wanaounga mkono Israel Maandamano Washington
Waandamanaji wanaounga mkono Israel na kupinga chuki dhidi ya Wayahudi wakijitokeza katika mitaa ya Washington Novemba 14, 2023.Picha: Leah Millis/REUTERS

Wizara ya Afya ya Gaza yasema idadi ya vifo imepita 15,900

Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel imepindukia 15,900, asilimia 70 wakiwa wanawake na watoto, na kwamba zaidi ya 42,000 wamejeruhiwa.

Wizara hiyo haitofautishi kati ya vifo vya raia na vya wanamgambo.

Hayo yakijiri, rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi wanatarajiwa kukutana mjini Moscow wiki hii.

Watakapokutana Alhamisi watabadilishana mawazo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kujadili mgogoro wa Ukanda wa Gaza.

Vyanzo: APTN, APTE, DPAE