1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yashambulia Khan Younis, kusini mwa Gaza

5 Desemba 2023

Israel imezidisha mashambulizi karibu na mji wa Khan Younis, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4ZnJ9
Zaidi ya robo tatu ya idadi jumla ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makaazi yao.
Zaidi ya robo tatu ya idadi jumla ya wakaazi wa Gaza wameyakimbia makaazi yao.Picha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Ving'ora vya magari ya wagonjwa vilisikika vikielekea katika hospitali ya mji huo kupeleka watu waliojeruhiwa kwenye awamu mpya ya mapigano hayo makali.

Ikiwa chini ya shinikizo la Marekani kuepusha maafa ya raia, Israel imesema inahakikisha usahihi wa shabaha kwenye mashambulizi yake huku ikitanua opereshani hiyo kusini mwa Gaza. Awali Israel ilifanya mashambulizi yake makubwa sehemu ya kaskazini mwa Gaza

Mashambulizi ya angani na vilevile ya ardhini, tayari yamesababisha robo tatu ya idadi jumla ya wakaazi milioni 2.3 wa ukanda huo kuyakimbia makaazi yao.

Katika hospitali ya Nasser wilaya ya Khan Younis, magari ya kuwabeba wagonjwa yaliwaleta makumi ya majeruhi usiku kucha. Katika kisa kimoja, mvulana mmoja alifikishwa hospitalini huku shati lake limelowa damu na mkono wake mmoja ukiwa umekatika kwa kulipuliwa. Huku akilia, Ibrahim al Najjar ambaye ni mmoja wa waathiriwa wa vita vya sasa vya Gaza eneo la Khan Younis amesema:

"Liko wapi shirika la Msalaba Mwekundu? yako wapi magari ya kubeba wagonjwa. Mume wangu na mtoto wangu wamekufa. Uko wapi Umoja wa Mataifa? Tangu saa nne usiku, watoto wangu bado wako chini ya vifusi, mimi nimeponea tu kimiujiza."

Makumi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa hospitalini usiku kucha kuamkia Jumanne 05.12.2023.
Makumi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa hospitalini usiku kucha kuamkia Jumanne 05.12.2023.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza inakaribia kuwa 'mbaya zaidi'

Picha za satelaiti zilizopigwa Jumapili zilionesha vifaru vya kivita vikiwa nje ya Khan Younis, mji ambao ndio sasa kitovu cha mashambulizi. Kabla ya vita mji huo ulikuwa na zaidi ya wakaazi 400,000.

Kama ilivyofanya katika operesheni yake ya kaskazini, Israel imewaamuru wakaazi wa karibu vitongoji 20 kuondoka badala ya eneo zima.

Wapalestina wasema hakuna mahali salama kukimbilia

Lakini kwa kuwa watu wengi waliokimbia kaskazini wamejazana kwenye kambi za wakimbizi za Umoja wa Mataifa zilizoko kusini na vilevile kwenye majumba binafsi, maeneo yaliyosalia kwa watu kukimbilia ni machache mno. Israel imewazuia watu waliokimbia vita kaskazini mwa Gaza kurudi.

Wapalestina wamesema Israel inapoendelea kulishambulia eneo hilo lililozingirwa, hakuna maeneo ambayo wanahisi kuwa salama. Wengi wanahofia kwamba wakiondoka majumbani mwao hawataruhusiwa kamwe kurudi.

Idadi ya waliofariki Gaza yaongezeka baada ya mapigano kuanza tena

Israel inasisitiza kuwa ni sharti iangamize kabisa miundo mbinu pana ya kijeshi ya Hamas, kundi ambalo pamoja na Marekani na Umoja wa Ulaya imeliorodhesha kuwa la kigaidi.

Israel na Hamas wameanza tena mapigano

Wanamgambo wa Hamas walifanya shambulizi la kigaidi la kushtukiza kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 na kusababisha vifo vya takriban watu 1,200 na kuwashika mateka takriban watu 240.

Guterres asikitishwa na kuanza upya kwa vita Ukanda wa Gaza

Kufuatia kisa hicho Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas. Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, hadi sasa zaidi ya Wapalestina 15,800 wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israel.

EU yahofia ongezeko la kitisho cha ugaidi

Kwingineko, kamishna wa masuala ya Ndani katika Umoja wa Ulaya Ylva Johansson, amesema umoja huo kwa sasa unakabiliwa na kitisho kikubwa cha ugaidi kutokana na vita vya Gaza.

Waislamu wajihisi hawako salama UIaya

Kamishna wa Masuala ya Ndani lkatika Umoja wa Ulaya, Ylva Johansson
Ylva Johansson atangaza kuongeza euro milioni 30 kwa ulinzi wa baadhi ya maeneo kama ya kuabudu.Picha: MENELAOS MYRILLAS/SOOC/AFP/Getty Images

Alipowasili katika mkutano wa mawaziri wa masuala ya ndani wa nchi wanachama wa umoja huo mjini Brussels mapema Jumanne, Johansson alisema mapigano kati ya Israel na Hamas yameendelea kusababisha mgawanyiko miongoni mwa jamii ya umoja huo. Na kwa kuzingatia msimu wa sikukuu unaokaribia, kuna kitisho kikubwa cha kufanyika mashambulizi ya kigaidi ndani ya Umoja wa Ulaya.

Miongoni mwa matukio aliyoyarejelea, Johansson alitaja kisa cha shambulizi la kisu mjini Paris siku ya Jumamosi ambapo mtalii Mjerumani aliuawa na wengine wawili walijeruhiwa.

Kamishna huyo alitangaza kuongeza euro milioni 30 kwa ulinzi wa maeneo kama ya kuabudu.

Mawaziri hao wanakutana kujadili hali ya usalama katika umoja wao kwa kuzingatia mzozo wa Mashariki ya Kati.

Soma makala zaidi kuhusu Mzozo wa Israel na Hamas

Vyanzo: APAE, DPAE