IDF yatanua mashambulizi ya ardhini Gaza
4 Desemba 2023Jeshi la Israel, IDF, limesema vikosi vyake vilikuwa vinakabiliana na wapiganaji wa Hamas kote katika Ukanda wa Gaza, katika ishara kwamba mapambano yake ya ardhini yalikuwa yameanza katika eneo la kusini walikorundikana wakimbizi, huku mashambulizi ya mabomu ya Israel yakiua na kujeruhi dazeni kadhaa za Wapalestina.
Mapambano hayo mapya yamefuatia kumalizika kwa mapatano ya siku saba ya kusitisha vita kati ya vikosi vya Israel na Hamas, ambayo yaliwezesha kubadilishana mateka 105 waliokuwa wanshikiliwa na Hamas, na wafungwa 240 wa Kipalestina.
Hamas ilisema jana Jumapili kwamba wapiganaji wake wamekabiliana na vikosi vya Israel umbali wa karibu kilomita mbili kutoka mji wa Khan Younis.
Soma pia: Israel yaamuru watu kuyahama maeneo zaidi Ukanda wa Gaza
Jeshi la Israel limechapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, ukiwa na amri mpya kwa wakazi wa Gaza kuondoka katika maeneo au majengo kwenye Ukandawa Gaza, kukiwa na mishale mitatu kwenye ramani inayoelekeza kusini, ikionesha mahali watu wanakopswa kwenda.
Hakuna eneo salama Gaza
Israel imesema inaainisha maeneo salama kwa raia wa Gaza ili kupunguza maafa kwao, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa na watu Gaza wanasema ni vigumu kutekeleza maagizo hayo kwa wakati kutoka na upatikanaji duni wa huduma za intaneti na umeme usiotabirika.
Afisa wa Hamas alieko mjini Lebanon alisema Jumapili kwamba hakuna maeneo salama Gaza.
Wakazi wamesema mashambulizi ya ndege na maroketi pia yalilenga hasa mji wa Khan Younis na mji mwingine wa Rafah kusini mwa Gaza, na kwamba hospitali zilikuwa zinapambana kuhudumia idadi kubwa ya majeruhi.
Mkazi wa Rafah, Abu Jahar al-Hajj, ambaye nyumba yake ilivunjwa kabisaa katika mashambulizi ya Israel, amezilaumu Marekani na Uingereza kwa yale yanayowakuta.
Soma pia: Israel na Hamas zapuuza miito ya kusitisha mapigano
"Wanatushambulia kwa mabomu makubwa, Marekani na Uingereza wanadhani sisi ya Muungano wa Kisovieti na tunataka kupigana nao, lakini sisi ni watu wasio na silaha, watu maskini; watoto wachanga, wanawake, wazee, hata wanyama na ndege hawakusazwa katika uharibifu huu," alsiema Al-Hajji.
Shinikizo laongezeka dhidi ya Israel
Msemaji wa jeshi la Israel Eylon Levy, alisema jeshi limeyashambulia maeneo zaidi ya 400 mwishoni mwa wiki, ikiwemo mashambulizi makubwa ya angani dhidi ya eneo la Khan Younis, na kwamba limeua wapiganaji wa Hamas na kuharibu miundombinu yao katika eneo la kaskazini la Beit Lahiya.
Israel iliapa kuisambaratisha Hamas kufuatia uvamizi wa wapiganaji wa kundi Oktoba 7 ambao ulisababisha vifo vya watu 1,200 kwa mujibu wa mamlaka za Israel, na wengine takribani 240 kuchukuliwa mateka.
Hata hivyo msemaji wa Jeshi la Israel amekiri kwamba jeshi hilo la IDF bado haliweza kuwashinda Hamas hata katika eneo la Kaskazini lilikoanzishia mashambulizi yake.
Soma pia: Mapigano makali yaanza tena Gaza baada ya mapatano kumalizika
Na wakati huo huo, shinikizo linazidi kwa Israel hata kutoka kwa mshirika wake mkuu Marekani, kupunguza vifo vya raia katika kamepni yake, huku kikisho cha kuongezeka kwa mzozo huo kikisalia pia kuwa kikubwa.
Mwishoni mwa wiki, waasi wa Kihouthi nchini Yemen wamezilenga kwa mashambulizi ya makombora ya masafa marefu meli za kibishara katika bahari ya Shamu, katika kile walichoeleza kuwa na kuwaunga mkono Wapalestina katika vita vyao na Israel.