Viongozi wakuu wa Ulaya wateua timu ya kuiongoza EU
28 Juni 2024Uteuzi wa von der Leyen ulikubaliwa siku ya Jumanne, lakini uamuzi rasmi ulichukuliwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels siku ya Alhamisi.
Kwenye mkutano wao wa kilele mjini Brussels, viongozi wakuu wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya pia waliwachagua waziri mkuu wa zamani wa Ureno Antonio Costa kuwa mwenyekiti ajaye wa Baraza la Ulaya, akirithi nafasi ya Charles Michel, na Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas kuwa mkuu ajae wa sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya, kuchukuwa nafasi ya Josep Borrell.
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel alisema maadili ya kidemokrasia na ushindani ni kati ya nguzo kuu za muhula mpya.
Soma pia: Umoja wa Ulaya kuwaidhinisha viongozi wakuu wa taasisi hiyo
"Pia tumedhamiria kuwa na ufanisi zaidi katikanyanja za ulinzi na usalama wa Ulaya. Katika suala la ulinzi wa Ulaya, tunataka kuanzisha miradi mikubwa, tunataka kushirikiana kutambua jinsi tunavyoweza kuhakikisha kuwa tunatoa msaada zaidi wa kifedha katika nyanja ya ulinzi," alisema Michel.
Kihunzi cha bungeni
Uidhinishaji wa viongozi wakuu hata hivyo haumaanishi uthibitisho wa muhula wa pili kwa von der Leyen bado. Anatakiwa kupata uungwaji mkono wa wajumbe walio wengi katika bunge la Ulaya lililochaguliwa hivi karibuni.
Viongozi wakuu wa Ulaya wanatumai muungano wa makundi matatu ya kisiasa utahakikisha uthibitisho wake, ukiakisi mirengo ya mawaziri wakuu na marais waliomuunga mkono kwenye Baraza la Ulaya.
Makundi hayo matatu ni kundi la von der Leyen mwenyewe la mrengo wa wastani wa kulia la European People's Party, EPP, kundi la mrengo wa wastani wa kushoto la Socialists and Democrats, S&D, pamoja na kundi la waliberali la Renewal Europe.
Mrengo mkali wa kulia walalamika kuachwa nje
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alishinikiza sana bila mafanikio, kupata moja ya nafasi za juu kwa ajili ya kundi la vyama vyenye mashaka na Umoja wa Ulaya la European Conservatives and Reformists, ECR, linalojumuisha chama chake cha mrengo mkali wa kulia cha Brothers of Italy, na ambalo lilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa Ulaya.
Meloni alisema kuachwa nje kwa ECR kwenye ugawaji wa nafasi za juu ilikuwa kwanza kabidaa kukosa heshima kwa raia wa Ulaya kwa sababu uteuzi huo haukuzingatia ongezeko la uungaji mkono wa vyama vya mrengo wa kulia katika uchaguzi.
Soma pia: Von der Leyen atetea kushirikiana na vyama vya mrengo wa kulia bungeni
Makundi ya EPP na S&D yalishika nafasi ya kwanza na ya pili katika uchaguzi huo, lakini kudi la Renewal lilishika nafasi ya nne nyuma ya ECR.
Baada ya mkutano huo, waziri mkuu wa Ubelgiji Alexander de Croo, aliliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba "siasa inastawi kwa watu wanaoungana na kufanya kazi pamoja, na siyo watu wanaosema nakwenda kuzuwia."