Viongozi wa EU wamteuwa von der Leyen kwa muhula wa pili
28 Juni 2024Hayo yamethibitishwa na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel. Uteuzi wa Von der Leyen ulifikiwa kimsingi Jumanne, lakini uamuzi rasmi ulifanywa Alhamisi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Chini ya mpango huo, waziri mkuu wa zamani wa Ureno Antonio Costa atakuwa rais ajaye wa Baraza la Ulaya, na Waziri Mkuu wa Estonia Kaja Kallas ameidhinishwa kuchukua wadhifa wa mkuu ajaye wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Uidhinishaji wa viongozi hao wa Umoja wa Ulaya haumaanishi muhula wa pili wa von der Leyen umethibitishwa. Bado anahitaji kupata uungwaji mkono wa wengi katika bunge jipya la Ulaya. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatumai kuwa muungano wa makundi matatu ya kisiasa utamthibitisha, na kuonyesha mirengo ya mawaziri wakuu na marais waliomuunga mkono katika Baraza la Ulaya. Makundi hayo matatu ni chama cha von der Leyen mwenyewe cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha European People's - EPP, cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Socialsts and Democrats - S&D na cha kiliberali cha Renew Europe.