Urusi yafanya shambulizi la makombora mjini Kyiv
21 Machi 2024Serhiy Popko, mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Ukraine, amesema shambulizi hilo la kwanza kubwa katika wiki za hivi karibuni lililenga mji huo wa Kyiv kwa makombora ya masafa marefu.
Popkov asema huduma za dharura zinaendelezwa Kyiv
Popko amesema baada ya kusitishwa kwa mashambulizi kwa siku 44, Urusi aliyoiita adui, ilifanya shambulizi lingine la kombora mjini humo na kwamba huduma zote za dharura zinafanya kazi katika eneo hilo kukabiliana na athari zake.
Soma pia:Ukraine yaishambulia Urusi na kuulenga mji mkuu Moscow na miundombinu muhimu
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko, amesema takriban watu 10 wamejeruhiwa kote mjini humo na kwamba msichana wa umri wa miaka 11, ni miongoni mwa watu wawili waliopelekwa hospitalini.
Jeshi la Ukraine ladungua makombora 31 ya Urusi
Jeshi la anga la Ukraine, limesema kuwa limedungua makombora 31 ya Urusiusiku kucha hili likiwa jaribio kubwa zaidi la mashambulizi baada ya wiki kadhaa wakati Urusi ikiapa kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni zaidi ya Ukraine katika maeneo yake ya mipaka.
Soma pia:Umoja wa Ulaya waonya juu ya mustakabali wa vita vya Ukraine
Katika taarifa kupitia mitandao ya kijamii, jeshi hilo la Ukraine limesema mashambulizi hayo yalikuwa yameelekezwa mjini Kyiv. Katika taarifa tofauti, wizara ya masuala ya ndani ya Ukraine, imesema kuwa takriban watu 13 walijeruhiwa katika mji huo mkuu.
Rais Zelensky atoa wito wa mshikamano wa kimataifa
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, leo ametoa wito kwa mataifa ya Magharibi kuonesha utashi wa kisiasa kulisaidia taifa hilo baada ya shambulizi hilo la Urusi mjini Kyiv.
Zelensky ameongeza kuwa matukio hayo yakutisha yanaendelea kila siku na kwamba inawezekana kukabiliana nayo na kuyamaliza kupitia mshikamano wa kimataifa.
Rais huyo pia ametoa wito kwa mataifa hayo ya Magharibi kupeleka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga nchini humo .
Viongozi wa Umoja wa Ulaya kuzungumzia vita vya Ukraine katika mkutano wao wa siku mbili
Katika hatua nyingine, marais na mawaziri wakuu wa mataifa ya Umoja wa Ulaya watakaokutana kuanzia leo mjini Brussels, watatafakari kuhusu mpango wa kutumia mapato yatokayo kwenye mali za Urusi zilizozuiwa barani Ulaya ili kununua silaha kwa ajili ya Ukraine.
Soma pia:EU kutumia fedha iliyotokana na mali ya Urusi iliyozuiwa kununua silaha na kuipa Ukraine
Pendekezo hilo lililowasilishwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo, Josep Borrell, litawezesha asilimia 90 ya mapato hayo kuwekezwa katika mfuko wa misaada ya kijeshi wa Umoja wa Ulaya ambao haukuzingatiwa katika bajeti yake na asilimia 10 iliyosalia kujumuishwa kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya ambayo itatumiwa katika kuongeza uwezo wa ulinzi wa Ukraine.
Soma pia:Marekani kuichangia Ukraine kijeshi dola milioni 300
Rais Zelensky atahutubia mkutano huo kwa njia ya video.
Mbali na hayo, shirika la habari la serikali ya Urusi TASS, limeripoti leo kuwa Urusi imewakabidhi watoto sita wa Ukraine kwa nchi yao katika hatua iliyosimamiwa na Qatar.