Urusi yadai kuviteka vijiji viwili mashariki mwa Ukraine
12 Januari 2025Urusi imedai kuchukua udhibiti wa vijiji viwili mashariki mwa Ukraine ambapo vikosi vyake vimekuwa vikisonga mbele kwa miezi kadhaa. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kundi la wanajeshi wa kusini, limeteka kijiji cha Yantarne katika eneo la mashariki la Donetsk, karibu kilomita 10 kusini magharibi mwa kituo kikuu cha usafirishaji cha Kurakhove, ambacho Moscow ilidai pia kukidhibiti wiki iliyopita.
Wizara hiyo ya ulinzi imeongeza kwamba wanajeshi wa Urusi pia wameteka kijiji cha Kalinove, kaskazini mashariki mwa mkoa wa Kharkiv. Siku ya Jumamosi pia, jeshi la Urusi lilitoa taarifa ya kudhibiti eneo jipya kaskazini magharibi mwa Kurakhove.Ukraine yaanzisha oparesheni mpya ya kijeshi Kursk
Kwa upande wake, jeshi la anga la Ukraine limedai kudungua ndege 60 za Droni za Urusi usiku wa kuamkia Jumapili. Vipande vya ndege hizo zilizoangushwa vimeharibu nyumba katika mikoa ya Kharkiv, Sumy na Poltava.