Ukraine yaanzisha oparesheni mpya ya kijeshi Kursk
7 Januari 2025Urusi ilipongeza kutekwa kwa mji wa Kurakvove ambao ni kitovu muhimu cha usafirishaji bidhaa huko mashariki mwa Ukraine. Moscow ilisema kudhibitiwa kwa mji huo kutawezesha vikosi vya Urusi kuteka kwa kasi kubwa eneo lote la mashariki la Donetsk. Lakini jeshi la Ukraine limesema mapigano bado yanaendelea Jumanne pembezoni mwa mji huo na kuishutumu Urusi kwa kutumia mbinu haramu za kijeshi.
Victor Tregubov, msemaji wa jeshi la Ukraine huko mashariki amesema wanajeshi wake wanashikilia viunga vya magharibi mwa mji wa Kurakvove. Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya mji imeharibiwa na Warusi ambao walikuwa wakiteketeza jengo moja baada ya jingine.
Tregubov alidai kuwa Ukraine ilikuwa ikiwapa hasara wanajeshi wa Urusi ili wasisonge mbele zaidi. Mji wa Kurakhove ulikuwa na idadi ya watu wapatao 18,000 kabla ya vita. Ni nyumbani kwa kituo cha umeme, na uko karibu na hifadhi kubwa ya madini ya lithiamu. Jeshi la Ukarine limesema bado linathibii kituo cha umeme cha mji huo.
Kila upande wajaribu kudhibiti maeneo mapya
Wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele katika eneo la mashariki la Donetsk -- ambalo Moscow ilidai kuliteka mwaka 2022 -- kwa miezi kadhaa. Pande zote mbili zinajaribu kupata maeneo mapya kabla ya Rais mteule wa Marekani Donald Trump kurejea madarakani baadaye mwezi huu.
Trump aliapa kurejesha amani ya haraka katika vita hivyo, vilivyodumu kwa takriban miaka mitatu, lakini hajaeleza mpango madhubuti.
Urusi ilisema Ukraine ilianzisha mashambulizi mapya katika eneo la mpakani la Kursk mwishoni mwa juma, miezi mitano baada ya jeshi la Kyiv dhibiti maeneo kumi na sita katika ardhi ya Urusi.
Kwenye jimbo la Kherson huko kusini mwa Ukraine, viongozi wa Urusi na Ukraine wanalauminia kwa mashambulizi yaliosababisha vifo vya raia wawili.
Huku hayo yakijiri, jeshi la Ukraine limetangaza kuanzisha oparesheni mpya za mashambulizi kwenye mkoa wa Kursk magharibi mwa Urusi. Makao makuu ya jeshi la Ukraine imetangaza kuishambulia Jumanne kamandi ya jeshi la Urusi katika mkoa huo wa Kursk.
Vikosi maalum vya Ukraine vilisema Jumanne viliwaua Wanajeshi 13 wa Korea Kaskazini wanaopigana kulisaidia jeshi la Urusi.