Urusi kuchukua jukumu la kusafirisha nafaka barani Afrika
24 Julai 2023Taarifa hiyo ya Putin iliyochapishwa kwenye tovuti ya Ikulu ya Kremlin imebaini kuwa Urusi itaendelea na juhudi zake kubwa za usambazaji wa nafaka, bidhaa za chakula, mbolea na bidhaa nyingine kuelekea barani Afrika.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Putin anatoa hakikisho kwamba Urusi ina uwezo wa kusawazisha kwa misingi ya kibiashara au hata bila malipo, nafaka za Ukraine.
Operesheni ya kijeshi ya Moscow ilizizuiabandari za Ukraine katika Bahari Nyeusi , kwa meli za kivita, hadi makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki na kutiwa saini mwezi Julai mwaka 2022 kuruhusu pia usafirishaji wa nafaka muhimu.
Mapema mwezi huu Urusi ilijiondoa katika mpango huo baada ya kulalamika kwamba makubaliano ya kuruhusu uuzaji wa bidhaa za chakula na mbolea za Urusi hayakuheshimiwa. Baadaye Moscow ilisisitiza kuwa itazichukulia meli za mizigo zinazosafiri kwenda Ukraine kupitia Bahari Nyeusi kama zenye uwezekano wa kulengwa kijeshi.
Soma pia: China yatoa wito wa kuanzishwa tena usafirishaji wa nafaka
Umoja wa Afrika umeelezea masikitiko yake juu ya uamuzi wa Moscow wa kusitisha mpango huo wa usafirishaji nafaka. Kulingana na Ikulu ya Kremlin, baadaye wiki hii Urusi itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa pili kati yake na Afrika pamoja na Jukwaa la Kiuchumi na Kibinadamu.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamesema Afrika inategemea pakubwa nafaka kutoka Urusi na Ukraine. Mpango huo wa nafaka mwaka jana uliwezesha mauzo ya zaidi ya tani milioni 32 za nafaka za Ukraine.
Mapigano yaendelea kuripotiwa
Hayo yakijiri, mapigano makali yameendelea kuripotiwa sehemu mbalimbali nchini Ukraine. Hata hivyo Ukraine imedai kuyashambulia kwa droni majengo mawili mjini Moscow huku Urusi ikisema itajibu vikali tukio hilo na mashambulizi mengine ya Kyiv katika rasi ya Crimea.
Moscow na Kyiv wameshutumiana kuishambulia kanisa kuu katika mji wa Odesa kunakoshuhudiwa mashambulizi makubwa yanayolenga bandari na miundombinu kadhaa. Leo hii pia, Urusi iliharibu kwa droni maghala ya nafaka ya Ukraine kwenye Mto Danube na kuwajeruhi watu sita.
Soma pia: Athari za uamuzi wa Urusi kujiondoa katika mpango wa usafirishaji nafaka
Urusi imeishutumu Kyiv kwa kufanya shambulio la makusudi dhidi ya waandishi wa habari katika mkoa wa kusini-mashariki mwa Ukraine wa Zaporizhzhia, ambapo mwandishi wa shirika la habari la serikali ya Urusi RIA Rostislav Zhuravlev ameuawa.
Wakati Urusi ikiapa kuwa itaendelea hadi kufikia mafanikio ya kile inachokiita "operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema hapo jana kuwa Ukraine imefanikiwa kurejesha na kuchukua udhibiti wa asilimia 50 ya eneo lake lililonyakuliwa na Urusi lakini akaonya kuwa bado ni mapema mno ili kufikia ushindi kamili.