Zelensky, Erdogan wazungumzia kufufua mkataba wa nafaka
22 Julai 2023Mkataba huo uliosambaratika baada ya Urusi kutangaza kujitoa, ulipatikana mwaka mmoja uliopita chini ya usimamizi wa Uturuki na Umoja wa Mataifa. Uliiruhusu Ukraine kuendelea kusafirisha shehena yake ya nafaka na mazao mengine kupitia bandari zake zililo kwenye Bahari Nyeusi.
Soma zaidi: Mkataba wa nafaka wafikia kikomo baada ya kujiondoa kwa Urusi
Akizungumza mjini Kiev baada ya mazungumzo hayo kwa njia ya simu na Erdogan, rais Zelensky amesema kufungua njia za kuendelea kusafirisha nafaka ni jambo lenye umuhimu mkubwa na ametaka ulimwengu ushirikiane kuepusha kile amekitaja kuwa "mzozo wa upatikanaji chakula duniani".
Uamuzi wa Urusi wa kujitoa kwenye mkataba huo mnamo Jumatatu ya wiki hii umesababisha mkwamo mpya wa shughuli za uchukuzi kwenye ujia wa Bahari Nyeusi. Moscow imeondoa jukumu la kuhakikisha usalama wa meli zinazopita kwenye eneo la Bahari Nyeusi lililo chini ya udhibiti wake.