1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Kongo waapa kufanya maandamano ya kupinga uchaguzi

27 Desemba 2023

Wagombea wa upinzani kwenye uchaguzi mkuu ambao matokeo yake yanasubiriwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamesema wataendelea na mipango yao ya kufanya maandamano hii leo licha ya katazo la serikali.

https://p.dw.com/p/4abFU
Uchaguzi wa Kongo
Uchaguzi wa Kongo Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Mmoja ya wagombea hao Martin Fayulu amesema wanasiasa wengine wote waliotishia kwa pamoja maandamanao makubwa kulaani dosari za uchaguzi huo mkuu uliofanyika Disemba 20 wataendelea na mipango hiyo kwa kuwa wanaamini uchaguzi huo ulijaa udanganyifu.

Fayulu amesema maandamano hayo yatafanyika kwa sababu upinzani hauwezi kukubali kile amekitaja kuwa "mapinduzi mengine kwa njia ya uchaguzi".

Amezungumza saa chache baada ya Naibu Waziri Mkuu wa Kongo, Peter Kazadi, kusema maandamano yanayopangwa na upinzani hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuvuruga kazi ya tume ya kuendelea kujumlisha matokeo.

"Hakuna serikali duniani itakayokubali hili, kwa hivyo hatutaruhusu litokee," Kizadi aliwaambia waandishi habari mjini Kinshasa na kuongeza kwamba upinzani unapaswa kusubiri matokeo kamili yatangazwe badala ya kufanya maandamano.

Rais Tshesekedi aongoza licha ya upinzani kuyapinga matokeo ya uchaguzi 

Wagombea vigogo uchaguzi wa Kongo, kutoka kushoto ni Moise Katumbi, Martin Fayulu na rais Felix Tshisekedi.
Wagombea vigogo uchaguzi wa Kongo, kutoka kushoto ni Moise Katumbi, Martin Fayulu na rais Felix Tshisekedi.

Tume ya Uchaguzi imekuwa ikitoa matokeo ya awali kwa ngazi ya urais yanayoonesha rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kwa idadi kubwa ya kura.

Matokeo ya uchaguzi mara nyingi huzusha machafuko nchini Kongo na kutishia kuliteteresha zaidi taifa hilo ambalo ni la pili kwa eneo barani Afrika na lenye utajiri mkubwa wa madini ya kinywe (Kobalti) na shaba lakini linaloandamwa na umasikini uliotopea na ukosefu mkubwa wa usalama upande wa mashariki.

Baada ya kampeni za uchaguzi, upigaji kura wa Disemba 20 ulikuwa wa mparaganyiko. Vifaa vya uchaguzi vilichelewa kwenye maeneo mengine, vilivyowasili vilishindwa kufanya kazi na sehemu ya wapiga kura hawakuyaona majina yao kwenye daftari lenye orodha.

Waandaaji maandamano ya leo Jumatano, wanailaumu tume ya uchaguzi kwa uamuzi wake wa kurefusha siu za kupiga kura kwenye vituo vilivyoshindwa kufunguliwa siku ya uchaguzi. Wanasema hilo ni kinyume cha katika na wanataka uchaguzi mzima urudiwe.

Baadhi ya waangalizi huru wa uchaguzi huo nao wamesema uamuzi wa tume ya CENI wa kuongeza siku za kupiga kura ´umeutia mchanga´ uhalali wa uchaguzi wenyewe.

CENI yakataa madai kuhusu uhalali wa uchaguzi baada ya kuongeza siku za kupiga kura 

Uchaguzi wa Kongo
Dosari nyingi ziliripotiwa uchaguzi wa Disemba 20 nchini Kongo Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

CENI imekiri kuwepo dosari za kuchelewa kuanza zoezi la upigaji kura mnamo Disemba 20 lakini imeyakataa madai ya uchaguzi huo kupoteza uhalali kwa kuongeza siku za watu kupiga kura.

Ilianza kuchapisha matokeo ya awali mwishoni mwa juma lililopita na hadi sasa rais Felix Tshisekedi anaongoza kwa wingi mkubwa wa asilimia 79 ya kura milioni 6.1 zilizokwishahesabiwa.

Anachuana na wagombea wengine 18 ikiwemo mfanyabiashara maarufu, Moise Katumbi, anayemfutia kwa asilimia 14 ya kura. Martin Fayulu yuko nafasi ya tatu akiwa na asilimia 4 kati ya kura zote zilizohesabiwa na matokeo yake kutangazwa.

CENI haijaweka wazi idadi ya watu walioshiriki uchaguzi huo wa wiki iliyopita ambao Wakongomani milioni 44 walikuwa na sifa za kupiga kura. Tume hiyo vilevile wala haijaashiria kura idadi ya kura zilizotangazwa matokeo yake zinafanya asilimia ngapi ya kura zilizopigwa.