DRC yapiga marufuku maandamano ya upinzani
26 Desemba 2023Siku ya Jumamosi, wagombea watano wa urais kutoka upinzani walimfahamisha Mea wa jiji la Kinshasa kuhusu nia yao ya kuandaa maandamano hayo.
Lakini serikali imesema maandamano hayataruhusiwa kwa kuwa matokeo ya uchaguzi bado hayajatangazwa rasmi. Waziri Mambo ya Ndani wa Kongo Peter Kazadi aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandamano ya kesho yanalenga kudhoofisha mchakato wa uchaguzi na serikali haiwezi kukubali hilo.
Viongozi wa upinzani walioitisha maandamano hayo ni pamoja na Martin Fayulu ambaye alidai alishinda uchaguzi uliopita mwaka wa 2018, na Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ambao wamekashifu uchaguzi huo na kuutaja kama kichekesho.
Soma pia: Marekani yatoa wito wa uwazi kwa uchaguzi wa Kongo
Moise Katumbi, mgombea mwingine na gavana wa zamani wa eneo la kusini-mashariki la Katanga, alitaka uchaguzi huo ubatilishwe. Takriban wapiga kura milioni 44, kati ya wakazi wapatao milioni 100 wa Kongo, walipiga kura ya kuchagua rais, wabunge, madiwani na viongozi wa manispaa katika kura za Jumatano iliyopita.