Uchaguzi Kongo: Tshisekedi aongoza kwenye matokeo ya awali
26 Desemba 2023Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo siku sita baada ya kufanyika uchaguzi mkuu uliogubikwa na kashfa za wizi wa kura na kucheleweshwa kusambazwa vifaa vya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, CENI, Denis Kadima amesema tume hiyo haitosita kubatilisha baadhi ya matokeo ya uchaguzi iwapo udanganyifu utathibitishwa.
Kadima amesema vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi hazikupangwa na CENI na amewatupia lawama baadhi ya wanasiasa ambao anasema walijaribu kuiba kura kwa kushirikana na baadhi ya mawakala wa tume ya uchaguzi.
Soma Pia:Upinzani Kongo wapanga kufanya maandamano kulalamikia kasoro za uchaguzi
Hadi Jumatatu 25.12.2023, baadhi ya maeneo yaliendelea kupiga kura, ikiwa ni siku tano baada ya uchaguzi kufanyika. Tume ya uchaguzi imesema hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wapiga kura wote kwenye maeneo ambako vifaa vya uchaguzi vilichelewa kufikishwa tarehe 20 Desemba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi, CENI mpaka sasa kura milioni 1.9, zimeshahesabiwa kati ya jumla ya wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha.
Soma Pia: Kongo yaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi
Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kulingana na matokeo hayo ya awali. Tshisekedi anafuatiwa katika nafasi ya pili na Moise Katumbi aliyekuwa meya wa jimbo la Katanga, yeye pia ni mfanyabiashara mkubwa.
Wagombea wengine wapatao 20 ikiwa pamoja na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Denis Mukwege wameshindwa kufikia asilimia 1 ya kura za awali.
Mpaka sasa tume ya uchaguzi,CENI haijabainisha viwango vya watu waliojitokeza kupiga kura lakini inaendelea kutoa matokeo hatua kwa hatua tangu siku ya Ijumaa.
Soma Pia:Mkuu wa Kanisa Katoliki Kongo ahimiza utulivu
Wapinzani wamelalamika juu ya vurumai na hitilafu, ambazo wanadai zimeutia dosari uchaguzi huo. Baadhi ya wapinzani wanapanga kufanya maandamano siku ya Jumatano 27.12.2023 na wengine wanataka uchaguzi wote ubatilishwe. Hata hivyo serikali ya Kongo imeyapiga marufuku maandamano hayo
Katika ujumbe wake wa Krisimasi, Askofu mkuu wa Dayosisi ya Kinshasa, Kadinali Fridolin Ambongo, ameuita uchaguzi huo kuwa ni vurumai kubwa.
Wakati huo huo hali ya mvutano imeongezeka mashariki mwa Kongo kutokana na mashambulio ya makundi yenye silaha.
Chanzo:AFP