UN yazindua mkakati mpya wa tabianchi
5 Juni 2020Chini ya kauli mbiu ya ''mbio za kuelekea kiwango sifuri'' juhudi hiyo mpya inanuwia kufanikisha lengo la kukomesha utoawaji gesi ukaa zinazochafua mazingira ifikapo mwaka 2050.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu kampuni 1,000, miji 458, vyuo vikuu 500, majimbo na mikoa 24 pamoja na wawekezaji wakubwa 36 wameridhia kuunga mkono pendekezo la kufikia kiwango sifuri cha utoaji gesi chafuzi kwa mazingira ifikapo 2050.
Miongoni mwa kampuni zinazojiunga na kampeni hiyo ni pamoja na Rolls-Royce, Nestle na kampuni kubwa ya mitindo ya Inditex. Zaidi ya nchi 120 duniani pia zimeridhia mpango huo wa kuwa na ulimwengu bila gesi chafuzi ifikapo katikati ya karne ya 21.
Haja ya mageuzi katika shughuli za kiuchumi
Rais wa mkutano ujao wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambaye pia ni waziri wa nishati wa Uingereza Alok Sharma, amesema hapo kabla kuwa shughuli za uchumi ulimwenguni zinapaswa kufanyiwa mageuzi ya kuwa endelevu na zisizochafua mazingira baada ya kumalizika kadhia ya janga la corona.
Shama amesema kampeni mpya ya Umoja wa Mataifa ya kufikia kiwango sifuri ni sharti izihimize kampuni na serikali duniani kuonesha nia ya kulinda mazingira na hali ya hewa.
Majanga ya asili yatokanayo na hali ya hewa yameonesha kile ambacho kinaweza kutokea duniani ikiwa kiwango cha joto katika uso wa sayari ya dunia hakitadhibitiwa.
Vimbunga kama vilivyotokea eneo la Afrika Mashariki, moto wa nyika uliozitia kishindo Australia na Marekani pamoja na kupungua kiwango cha barafu kwenye ncha mbili za ulimwengu ni kati ya madhara yatakayojitokeza.
Kulingana na jukwa la mabadiliko ya tabia nchi la Umoja wa Mataifa, kiwango cha jto katika uso wa dunia kimepanda kwa nyuzi moja ikilinganishwa na kabla ya enzi ya mapinduzi ya viwanda na kwamba miaka minne iliyopita imekuwa na hali ya joto kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.
Kenya yapiga marufuku
Katika hatua nyingine Kenya imepiga marufuku matumizi ya plastiki kama vile chupa za maji na mirija katika mbuga zake za wanyama, fukwe na misitu na maeneo mengine yanayohifadhiwa.
Utekelezaji wa marufuku hiyo iliyotangazwa mwaka mmoja uliyopita, umeagizwa kupitia barua kutoka kwa waziri wa utalii Najib Balala wiki iliyopita, na unaanza hii leo, miaka minne tangu Kenya ilipotangaza moja ya marufuku kali zaidi duniani kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki.
Shirika la programu ya mazingira za Umoja wa Mataifa UNEP, linakadiria kwamba zaidi ya tani milioni 8.3 za plastiki zimezalishwa kila mwaka duniani tangu mwanzoni mwa miaka ya 1950, ambapo karibuni asilimia 60 inaishia kwenye madampo au mazingira ya asili.
UNEP imesema katika taarifa kwamba kwa kupiga marufuku plasitiki za matumizi ya mara moja kwenye mbuga za taifa na maeneo yanayohifadhiwa, Kenya imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kushughulikia janga na dunia la uchafuzi wa plastiki.
Chanzo: Mashirika