UN yaishtumu Uganda kuwasaidia waasi wa M23
10 Julai 2024Ugandaimekanusha kuhusika katika mzozo huo, ikisema inashirikiana kwa karibu na vikosi vya serikali ya Kongo. Kwa muda mrefu Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kuunga mkono kundi la M23, ambalo mara kadhaa limeteka ardhi kubwa ya eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo, madai ambayo Rwanda ilikanusha.
Kongo imekumbwa na vita kwa miongo kadhaa. Uganda na Rwanda ziliivamia mwaka 1996 na 1998 kwa kile walichosema ni kujilinda dhidi ya makundi ya wanamgambo wa ndani. Uganda bado inaendesha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa Kongo dhidi ya kundi la waasi la Uganda, na Allied Democratic Forces,ADF.
Soma pia: Waasi wa M23 waendelea kukamata miji muhimu ya Kongo
Waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi wamekuwa wakianzisha uasi mpya katika eneo la mashariki mwa Kongo linalokumbwa na uasi tangu 2022.
Wanajeshi wa Uganda walikuwa sehemu ya kikosi cha kikanda kilichotumwa mnamo Novemba 2022 kusimamia usitishaji mapigano na M23. Serikali ya Kongo ilitoa wito kwa kikosi hicho kuondoka mwaka jana, ikisema hakikuwa na ufanisi.
"Tangu kuzuka upya kwa mzozo wa M23, Uganda haijazuia kuwepo kwa wanajeshi wa M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) kwenye ardhi yake au kupita humo," lilisema kundi la Wataalamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika ripoti yao iliyotumwa kwa kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama mwishoni mwa Aprili na kisha kwa wajumbe wa Baraza la Usalama mwezi Juni.
Kundi hilo la Umoja wa Mataifa pia lilisema limepata ushahidi unaothibitisha uungaji mkono hai wa M23 na jeshi la Uganda na maafisa wa ujasusi wa kijeshi, huku viongozi wa M23, akiwemo Sultani Makenga aliyewekewa vikwazo, wakisafiri kwenda Uganda kuhudhuria mikutano.
Jeshi la Uganda lakanusha madai ya UN
Naibu msemaji wa jeshi la Uganda, Deo Akiiki, alisema katika mazungumzo na shirika la habari ya Reuters kuwa ripoti kama hizo zinalishutumu jeshi la nchi hiyo ya Afrika Mashariki wakati uhusiano wake na vikosi vya Kongo (FARDC) uko katika kiwango bora.
"Itakuwa uenda wazimu kwetu kuvuruga eneo lile lile tunalojitolea kila kitu kuhakikisha lina utaulivu," alisema Akiiki.
Ripoti hiyo ya UN ilisema wanajeshi 3,000-4,000 wa Rwanda walikuwa wakipigana upande wa waasi wa M23 dhidi ya jeshi la Kongo. "Udhibiti wa ukweli na mwongozo wa jeshi la Rwanda juu ya operesheni za M23 pia unaifanya Rwanda kuwajibika kwa hatua za M23," walisema wataalam wa Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Tshisekedi azidi kutema cheche dhidi ya Rwanda, M23 washambulia tena Sake
Katika majibu yake, Rwanda ilisema Kongo ilikuwa ikifadhili na kupigana pamoja na waasi wa Kihutu, wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), ambao wameshambulia Watutsi katika nchi zote mbili.
"DRC ina uwezo wote wa kupunguza mzozo huu ikiwa wanataka, lakini hadi wakati huo Rwanda itaendelea kujilinda," msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo aliiambia Reuters.
Chanzo: Reuters