UN: Raia 440 waliuwawa katika mapigano Sudan Kusini
1 Machi 2022Ripoti hiyo ya pamoja iliyotolewa na ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini na shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa imeonesha, ukiukwaji mkubwa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya mamia ya raia wakati wa mapigano katika kaunti ya Tambura, jimbo la Equatoria Magharibi.
Ripoti imewalaumu zaidi wanajeshi wanaomtii Rais Salva Kiir na wapinzani katika Vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan/Jeshi la Upinzani (SPLM/A-IO) la Makamu wa Rais Riek Machar, pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana nao katika ghasia hizo.
Kati ya Juni na Septemba mwaka jana, takriban raia 440 waliuawa katika mapigano kati ya makundi hasimu katika kaunti ya Tambura, 18 kujeruhiwa na 74 kutekwa nyara, ripoti imebaini.
Soma zaidi: Sudan Kusini yapuuza ripoti ya UN kuhusu ufisadi wa wanasiasa wake
Takriban raia 64 pia walikabiliwa na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro, miongoni mwao ni msichana wa miaka 13 ambaye alibakwa na genge hadi kufa, sehemu ya ripoti ilibainisha, huku watu wasiopungua 56 wakiripotiwa kutoweka katika kipindi cha Juni hadi Septemba.
Ripoti imeongeza kuwa takriban watu 80,000 walilazimika kukimbia makaazi yao ili kutoroka mapigano.
Uporaji na uharibifu wa mali, usajili wa watoto, mashambulizi dhidi ya wafanyakazi, matamshi ya chuki na uchochezi wa vurugu ni miongoni mwa ukiukwaji wa haki za binadamu ambao uchunguzi ulibaini.
Waathirika: waliofanya uhalifu walificha utambulisho wao
Idadi kubwa ya mashahidi na waathirika wa machafuko waliohojiwa katika ripoti hiyo "walionyesha wanaume waliojihami na bunduki aina ya AK-47 pamoja na silaha zingine za kijadi yakiwemo mapanga, visu na marungu.
Washambuliaji mara nyingi walihamia katika vikundi vidogo, wakiwa wamevalia nguo nyeusi, walificha nyuso zao na walizungumza mseto wa lugha ikiwemo Azande, Balanda na Kiarabu. Mashahidi walinukuliwa na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Mkoa wa Tambura, ambao hauko mbali na mpaka na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa muda mrefu umekuwa uwanja wa mapambano kati ya makabila ya Azande na Balanda.
Soma zaidi:Mchakato wa amani unaoyumba Sudan Kusini wawasikitisha raia
Ripoti hiyo imewashutumu maafisa wa ngazi za juu katika jeshi, jamii na hata viongozi wa dini kwa uchochezi wa wazi na kuanzisha wa ghasia zilizozuka hivi karibuni katika eneo la Tambura.
UN: waliohusika wachukuliwe hatua
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet alitoa wito kwa pande zote katika mzozo huo kuwawajibisha watu wote wanaohusishwa na uvunjaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji, ubakaji na utekaji nyara.
" wahusika wa unyanyasaji huo wa kikatili dhidi ya binadamu Sudan Kusini lazima kuadhibiwa" Aliongeza Bachelet katika taarifa yake iliotolewa leo Jumanne.
Taifa hilo lililopo kusini mwa jangwa la Sahara, limekumbwa na ukosefu wa utulivu wa kudumu tangu kujipatia uhuru wake mwaka 2011, ikiwa ni pamoja na vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kati ya vikosi vinavyomtii Kiir na Machar ambavyo viligharimu karibu maisha ya watu 400,000.
Soma pia:Amnesty: Vita vya Sudan vinaweza kuwa uhalifu wa kivita
Miaka miwili iliyopita mahasimu hao wawili waliunda serikali ya umoja, wakiimarisha mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018 ambao ulimaliza mzozo huo.
Lakini tangu wakati huo,imekuwa ikikabiliana na mambo kadha wa kadha ikiwemo majanga mbalimbali kama vile mafuriko, njaa, pamoja na ghasia za kisiasa huku viongozi hao mahasimu wakishindwa kutekeleza masharti muhimu katika makubaliano hayo ya amani.
Wasiwasi wa taifa hilo kurejea kwenye mzozo
Ikiwa imesalia mwaka mmoja taifa hilo changa kabisa ulimwenguni kuingia katika uchaguzi, wameshindwa kuunda kamandi ya umoja wa Kijeshi, ikiwa ni kipengele muhimu katika makubaliano ya amani.
Kufuatia kushindwa kwa utekelezwaji wa masharti hayo muhimu Yasmin Sooka mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini ameonya kuwa kuna hatari ya taifa hilo kurejea kwenye mzozo.
Chanzo: AFP