Mchakato wa amani Sudan Kusini hatarini: UN
8 Desemba 2021Onyo hilo linatokana na kujikokota kwa hatua zinazopigwa kufanikisha mchakato wenyewe. Umoja huo umetoa wito wa kuanzishwa haraka mazungumzo mapya.
Umoja wa Mataifa umewaonya viongozi wa Sudan Kusini kuwa mchakato dhaifu wa amani katika taifa hilo changa upo katika hatari kubwa kutokana na kujikokota kwa hatua zinazopigwa na kutoa wito wa kuanzishwa haraka mazungumzo mapya.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini Nicholas Haysom amesema mchakato huo wa amani unakabiliwa na kitisho cha kutotekelezeka kama hautaendeshwa kwa kasi.
Makubaliano ya amani ya mwaka wa 2018 yaliyomaliza vita yamegubikwa na ugomvi kati ya pande pinzani, na vipengele muhimu vya mkataba huo bado havijatekelezwa.
Haysom pia ametahadharisha kuhusu mzozo mkubwa wa mafuriko nchini humo, ambao umewaathiri watu zaidi ya 800,000 kufuatia miezi sita ya mvua kubwa.
Amesema hali ni mbaya kwa sababu maji ya mafuriko bado hayajapungua na mamia kwa maelfu ya watu bado hawana makazi na wanahitaji msaada wa dharura.