UN: Mwaka 2023 ulikuwa mbaya kwa wahamiaji
7 Machi 2024Idadi ya vifo vya mwaka jana ikiongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Katika ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumatano, IOM imesema kwamba zaidi ya wahamiaji 8,500 walikufa mwaka jana duniani kote katika njia wanazotumia wahamiaji za ardhini na majini. Hiki ni kiwango cha juu zaidi tangu shirika hilo lilipoanza kuhesabu vifo vya wahamiaji muongo mmoja uliopita.
Soma pia: UN: Zaidi ya wahamiaji 180,000 wamevuka bahari ya Mediterania na kuingia Ulaya mwaka 2023
Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva, Uswisi, limetahadharisha kuwa kuna uwezekano kwamba hali halisi huenda ni mbaya zaidi, kwa kuzingatia kwamba si kila muhamiaji aliyepoteza maisha aliweza kupatikana taarifa zake katika ukusanyaji wa data.
Ongezeko la vifo Asia
Kwa ujumla, idadi kubwa zaidi ya vifo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa barani Asia, ambako zaidi ya wahamiaji 2,000 walikufa ikilinganishwa na wastani wa kila mwaka wa chini ya 1,000 tangu 2014.
Kupitia barua pepe, msemaji wa IOM, Jorge Galindo, amesema ongezeko la vifo barani Asia mwaka jana lilitokana na vifo miongoni mwa Waafghani wanaokimbilia maeneo jirani kama Iran pamoja na wakimbizi wa Rohingya kwenye njia za baharini.
Aidha shirika hilo limeongeza kwamba idadi kubwa ya vifo vya wahamiaji, lilitokea kwenye njia hatari ya kuvuuka Bahari ya Mediterenia na kuonesha umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kupoteza zaidi maisha ya watu.
Idadi hiyo pia inajumuisha wahamiaji waliotoweka ambao mara nyingi wanajaribu kuvuuka bahari na kusadikiwa kuwa walikufa hata ikiwa miili yao haikupatikana.
Soma pia: UN: Vifo ya wahamiaji wanaovuka bahari kuelekea bara Ulaya vyaongezeka maradufu
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Ugochi Daniels, amesema kwamba takwimu hizo za kutisha zilizokusanywa na Mradi wa Wahamiaji Waliopotea pia ni ukumbusho kwamba kuna haja ya kuhakikisha uhamiaji salama kwa wote, ili miaka kumi kutoka sasa, watu wasilazimike kuhatarisha maisha yao katika kutafuta maisha bora.
IOM imesema kuwa ukosefu wa njia salama zilizodhibitiwa hulazimisha maelfu kuchukua njia hatari za uhamiaji.
Aidha ripoti hiyo imesema kwamba njia hatari zaidi kwa wahamiaji ni kupitia Bahari ya Mediterania, ambayo iliripotiwa kuwa na vifo vya wahamiaji 3,129 mnamo 2023 wakati walipokuwa wakijaribu kuvuuka kuingia Ulaya kutoka Afrika Kaskazini. Hiki ni kiwango kikubwa kabisa cha vifo katika njia hii tangu 2017.
dpa