1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waomba usalama wa nyuklia kuangaziwa

7 Machi 2022

Umoja wa Ulaya umeliomba shirika la kimataifa la kudhibiti nguvu za atomiki kuhakikisha usalama wa vinu vya nyuklia nchini Ukraine ambavyo viwili miongoni mwake vinadhibitiwa na Urusi.

https://p.dw.com/p/486x5
Symbol der IAEA in Wien
Picha: Sascha Steinach/dpa/picture alliance

Umoja huo umeliomba shirika hilo la kudhibiti nguvu ya atomiki la IAEA pia kuomba msaada wa jumuiya ya kimataifa iwapo kutatokea dharura yoyote. Mwito huu unatolewa wakati mzozo kati ya Urusi na Ukraine ukiendelea kuibua wasiwasi ndani ya nje ya mipaka ya Ukraine.

Soma Zaidi: Mtambo wa nishati ya nyuklia washambuliwa Ukraine

Sehemu ya barua iliyoandikwa na mkuu wa masuala ya nishati wa Umoja wa Ulaya Kadri Simson na kuonwa na shirika la habari la Reuters ilisema na hapa nanukuu "Mimi.. ninaomba IAEA kufanya kila linalowezekana kuhakikisha usalama wa nyuklia katika maeneo ya nyuklia ya Ukraine katika mazingira ya sasa ya vita". Barua hii iliandikwa kwa mkurugenzi wa IAEA Rafael Grossi, Machi 4.

Ikumbukwe kwamba Urusi inakidhibiti kinu kikubwa kabisa cha nyuklia barani Ulaya, kilichopo Ukraine cha Zaporizhzhia na eneo la Chernobyl ambako ajali mbaya kabisa ya nyuklia ilitokea mwaka 1986. Tangu ilipovikamata Urusi imekuwa ikiviendesha na kuzuia mawasiliana kutoka nje, limesema shirika hilo la IAEA jana Jumapili na kusema lina wasiwasi mno na hatua hiyo.

Nchini Ukraine kwenyewe, Urusi imetangaza njia mpya na salama za raia wa Ukraine kupita mapema leo. Raia hao ni waliokuwa wamekwama kutokana na mashambulizi yake ya mabomu nchini humo akishirikiana na Belarus. Hata hivyo hatua hiyo imepuuziliwa mbali na Ukraine.

Krieg in der Ukraine I Mariupol
Mji wa Mariupol umekabiliwa na mashambulizi ya Urusi na baadae kufunguliwa njia salama ya raia kupita. Hata hivyo makubaliano ya kwanza hayakudumu.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Tangazo hilo linatolewa siku mbili baada ya jaribio la kwanza la kusitisha mapigano ili kuruhusu raia kuondoka katika mji uliozingirwa wa Mariupol  kushindikana. Njia mpya zilizotangazwa na Urusi zingefunguliwa majira ya saa moja kwa saa za Urusi kuanzia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na majiji ya mashariki ya Kharkiv na Sumy pamoja na Mariupol, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi.

Ramani iliyotolewa inawalekeza raia kutoka Kyiv kuelekea Belarus, wakati wale wanaotoka Kharkiv wataruhusiwa kwenda Urusi tu lakini pia imesema itatoa usafiri wa ndege zitakazowachukua raia wa Ukraine kuwapeleka nchini humo, kutokea Kyiv.

Soma Zaidi: Maoni: Msaada wa NATO na Magharibi kwa Ukraine hautoshi

Msemaji wa rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ameiita hatua hiyo isiyo ya maadili kabisa na kusema Urusi inajaribu kuwatumia watu wake wanaoteseka kuandaa picha za kuonyeshwa kwenye televisheni. Amesema hili ni moja ya matatizo yanayochangia makubaliano ya njia hizo kuvunjika.

Huku hayo yakiendelea, shirika la Msalaba Mwekundu nchini China limeahidi kutoa misaada ya kiutu nchini Ukraine haraka iwezekanavyo hii ikiwa ni kulingana na waziri wa mambo ya nje Wang Yi. Ingawa China imekataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lakini bado inasifu ushirikiano wake na taifa hilo ikisema bado uko imara na kusema itaendeleza juhudi za kusuluhisha mzozo wa kibinaadamu nchini Ukraine.

Mwanadiplomasi wa juu katika Umoja wa Ulaya Josep Borrel amenukuliwa leo akisema iwapo Urusi itaendeleza mashambulizi ya mabomu nchini Ukraine ni dhahiri kwamba raia wengi watalikimbia taifa hilo na kuongeza kuwa wanalazimika kujiandaa kupokea wakimbizi karibu milioni 5 huku akiyatolea mwito mataifa wanachama kujiandaa kirasilimali ili kusaidia mataifa yatakayowapokea.

Mashirika: RTRE