Juhudi za kuwahamisha wakaazi wa Mariupol zashindwa tena
6 Machi 2022Kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC imesema hayo Jumapili mnamo wakati raia katika mji huo wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha. ICRC imesema jaribio hilo la pili lililenga kuwahamisha takriban wakaazi 200,000.
Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine yapindukia milioni 1.5, UN
Kamati hiyo imesema kufeli mara mbili kwa juhudi hizo kunaonesha ukosefu wa makubaliano ya msingi kati ya pande mbili husika kwenye mgogoro huo.
"Ili kuwepo njia salama ya kiutu kwa wakaazi kuhamishwa, sharti kuwepo hali ya juu ya kuaminiana kati ya pande mbili husika kwenye mzozo, si kwa- maneno tu bali kwa maelewano mapana na marefu," imesema ICRC.
Putin ailaumu Ukraine kwa kufeli kwa juhudi za kuwaondoa raia Mariupol
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameilaumu Ukraine kufuatia kufeli kwa juhudi za kuwaondoa raia katika mji huo unaozingirwa na wanajeshi wa Urusi.
Urusi yazidisha mashambulizi katika miji ya Ukraine
Kwenye mazungumzo yake na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa njia ya simu, Putin alisema Ukraine imeshindwa kutimiza ahadi ambazo zimewekwa kwenye makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano ili kuwezesha juhudi za kiutu. Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Urusi.
Putin alisema watu wenye siasa za kizalendo wa Ukraine waliwazuia raia pamoja na raia wa kigeni kuondoka katika mji huo na mji mmingine jirani wa Volnovakha licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mashambulizi.
"Na waliutumia muda huo wa kusitisha mashambulizi kuongeza vikosi vyao na upinzani katika maeneo yao," Putin alimwambia Macron.
Marekani au Urusi? Mzozo wa Ukraine waiweka njia panda Ghuba
Alisema pia kuwa vikosi vya Urusi vinakidhibiti kituo cha nishati ya nyuklia Chernobyl.
"Haya yote yanafanywa ili kuzuia uchokozi wowote unaoweza kufanywa na Wanazi mamboleo na magaidi wa Ukraine na kusababisha athari mbaya," Urusi imesema.
Kulingana na taarifa kutoka ikulu ya rais nchini Ufaransa, marais hao walizungumza kwa muda wa jumla ya saa moja na dakika 45.
Tayyip Erdogan amtaka Putin kusitisha mashambulizi mara moja
Naye rais wa uturuki Tayyip Erdogan amemhimiza Vladimir Putin kusitisha mashambulizi nchini Ukraine, afungue njia za kutoa misaada ya kiutu na asaini makubaliano ya amani, ofisi yake imesema.
Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, inapakana na Urusi na vilevile Ukraine katika Bahari Nyeusi na ina uhusiano mzuri na nchi zote mbili.
Uturuki imeutaja uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine kuwa jambo lisilokubalika na imejitolea kuwa mpatanishi. Hata hivyo inapinga vikwazo dhidi ya Urusi.
Kwenye taarifa baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Putin kwa muda wa saa moja, ikulu ya rais Uturuki imesema, Erdogan amemwambia Putin kwamba Uturuki iko tayari kushiriki juhudi za kusaka suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya amani.
"Rais Erdogan alisema kusitishwa kwa mashambulizi kutawezesha kuondoa wasiwasi wa kiutu katika kanda hiyo, na kutatoa nafasi ya suluhisho la kisiasa." Ofisi ya Erdogan imeongeza.
Kremlin imesema Putin alimwambia Erdogan kwamba Urusi itasitisha tu operesheni yake ya kijeshi ikiwa Ukraine itaacha mapambano na ikiwa masharti ya Urusi yatekelezwa.
Urusi yawashikilia waandamanaji 2,500
Katika tukio jingine, Urusi imewakamata waandamanaji 2,500 siku ya Jumapili waliokuwa wakiandamana kupinga uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, siku 11 tangu uvamizi huo kuanza.
Msemaji wa polisi amesema watu 1,700 wamekamatwa Moscow baada ya takriban watu 2,500 kushiriki "maandamano ambayo hayakuidhinishwa" na kwamba wengine 750 walikamatwa wakati waandamanaji 1,500 walijitokeza katika mji wa pili kwa ukubwa Saint Petersburg. Shirika la habari la Urusi limeripoti.
Shirika la haki za binadamu linalofuatilia ukamataji unaofanywa dhidi ya waandamanaji wa upinzani nchini Urusi, limesema watu 2,575 wamekamatwa katika jumla ya miji 49 nchini Urusi.
Svetlana Gannushkina, mwanaharakati nguli wa haki za binadamu na ambaye amepigiwa upatu kushinda tuzo ya Nobel, ni miongoni mwa walioshikiliwa na polisi, siku ambayo alikuwa akisherehekea miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Ukamataji wa waandamanaji siku ya Jumapili unafikisha jumla ya waandamanaji waliokamatwa kupita 10,000 tangu Februari 24, wakati rais Putin alipowaamuru wanajeshi wake kuvamia Ukraine.
(AFP, RTR)