Umoja wa Mataifa waionya Israel juu ya kuizingira Hamas
10 Oktoba 2023Siku nne baada ya Hamas wa Palestina kuishambulia Israel, jeshi la Israel limesema uzio wa mpaka na Gaza sasa uko salama, wakati zoezi la kuwahamisha watu wa jamii za Israeli wanaoishi karibu na mpaka likiendelea.
Jeshi la Israel, IDF limesema limechukua tena udhibiti wa uzio wa mpaka wa Gaza baada ya uvamizi wa hamas mwishoni mwa wiki ilyiopita. Kulingana na maoni yaliyorushwa na kituo cha Radio ya Jeshi la Israel na kunukuliwa na shirika la habari la Reuters, msemaji mkuu wa jeshi Daniel Hagari alisema vikosi vya Israel vinatega mabomu ya ardhini katika maeneo ambako uzio ulivunjwa.
Aliongeza kuwa tangu jana Jumatatu hakukua na uvamizi mpya kutoka Gaza kunakotawaliwa na Hamas na kuongeza kuwa IDF linazidi kujiimarisha kwenye eneo hilo dhidi ya uvamizi wa aina yoyote.
"IDF imedhibiti kikamilifu eneo linalozunguka Ukanda wa Gaza. Hakukuwa na uvamizi wowote wa magaidi usiku wa kuamkia leo, kulingana na kile tunachokijua. Sera yetu ya kufyatua risasi kuelekea kwenye uzio inamaanisha kwamba mtu yeyote anayekaribia uzio huo atauawa."
Soma pia: Ni lipi kusudio la Hamas kuwachukua mateka raia wa Israel?
Katika hatua nyingine, mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk ameonya kupitia taarifa yake kwamba mizngiro kamili wa vikosi vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza umezuiwa chini ya sheria ya kimataifa, kwa kuwa unawaweka watu hatarini kwa kuwazuia raia kufikiwa na huduma za msingi. Turk alikuwa akijibu tangazo la waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant ya kwamba wamezingira Ukanda wa Gaza.
Turk aidha amesema mapema leo Israel imeshambulia majengo ya makaazi pamoja na shule na majengo ya Umoja wa Mataifa kote kwenye eneo hilo na kusababisha majeruhi, hii ikiwa ni kulingana na taarifa zilizokusanywa na ofisi yake.
Umoja wa Mataifa umesema mapema leo kwamba karibu watu 200,000 wameyakimbia makazi yao na wengine wanakabiliwa na uhaba wa maji na umeme kutokana na mzingiro.
Soma pia: Serikali ya Israel yawaamuru wanajeshi wake kulizingira eneo la Ukanda wa Gaza
Israel aidha imesema imepeleka vifaru kwenye mipaka na Lebanon katikati ya wasiwasi wa kuongezeka kwa mzozo baada ya kuishambulia Lebanon na kuwaua karibu wanamgambo watatu wa Hezbollah jana Jumatatu.
Na huko Muscat, hii leo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakikutana kwenye mkutano usio wa kawaida kujadiliana juu ya kuzuia misaada ya kifedha kwenye maeneo ya Palestina. Misaada ya Umoja wa Ulaya inafikia kiasi cha yuro milioni 691.
Ujerumani ni moja ya mataifa yanayolitaja kundi la Hamas kuwa la kigaidi
Umoja huo, Ujerumani na Marekani na baadhi ya mataifa wanalichukulia kundi la Hamas kuwa ni la kigaidi.
Kabla ya mkutano huo wa leo, kaimu waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Jose Manuel Albares amesema watapinga hatua yoyote ya kusimamishwa kwa malipo ya fedha kwa Wapalestina, akisema haina tija. Amesema hakuna sababu ya kuwachanganya Hamas wanaotajwa kuwa kundi la kigaidi na Wapalestina ama Mamlaka ya Palestina ama hata mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Palestina. Ufaransa pia imesema haitaunga mkono hatua hiyo.
Huku hayo yakiendelea, Iran kwa mara nyingine imekana kuhusika na shambulizi la Hamas. Kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema hawahusiki kwa namna yoyote licha ya mahusiano baina yao na kundi hilo.
Soma pia: Baada ya shambulio la Hamas, Netanyahu asema Israel iko vitani
Aidha, taarifa kutoka Berlin zinasema Ujerumani, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zimeahidi kusimama pamoja na Israel kufuatia shambulizi hilo la Hamas. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kupitia ukurasa wake wa X kwamba mataifa hayo matano yatahakikisha Israel inaweza kuwalinda na raia wake dhidi ya mashambulizi mabaya, pamoja na kulilaani tukio hilo la Jumamosi.