Ni lipi kusudio la Hamas kuwachukua mateka raia wa Israel?
10 Oktoba 2023Katika shambulio la kutisha la siku ya Jumamosi ambapo kundi la kipalestina la Hamas lilivamia miji ya Israel na kuwaua Waisraeli wapatao 800 na kuondoka na makumi ya mateka, Israel inakabiliana na mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu vita vya mwaka 1973.
Netanyahu ameapa "kulipiza kisasi" lakini hatima ya Watu wa Israel waliofanywa mateka na kupelekwa hadi Gaza ikiwa ni pamoja na askari, wazee, wanawake na watoto na ambao idadi yao bado haijulikani, inaiweka katika wakati mgumu Israel kutimiza ahadi yake ya kulipiza kisasi kwa haraka na uthabiti. Tel Aviv inatakiwa pia kuheshimu kanuni yake ya muda mrefu ya kutomwacha raia yoyote katika matatizo.
Waisraeli wamejawa na hofu kutokana na shambulio hilo la Hamas lakini pia kutokana na picha zinasosambazwa mitandaoni zinazowaonesha wayahudi wakilazimishwa kuelekea Gaza.
"Sidhani kama watarudi," alisema msichana mmoja wa Kiisraeli huku akiwa analia. Dada yake aliuawa katika shambulio hilo huku yeye na wazazi wake wakishikiliwa mateka. Alionyeshwa kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa X na Afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Balozi David Saranga.
Historia ya kubadilishana wafungwa
Mnamo mwaka 2011, Israel iliwakabidhi mamia ya wafungwa wa Kipalestina ili kuachiliwa tu kwa mwanajeshi mmoja wa Israel, Gilad Shalit, ambaye alikuwa akishikiliwa kwa miaka mitano.
Zoezi hilo la kubadilishana wafungwa ambalo wakati huo lilikosolewa hadi na baadhi ya Waisraeli wenyewe kwa kusema halikuwa na usawa, linaonekana mara hii kutowezekana wakati makumi ya waIsrael huenda wameshikiliwa na kundi la Hamas. Israel imekuwa na sera ya kuhakikisha inawalinda raia wote na hasa kutomwacha mateka yeyote hatarini.
Soma pia: Guterres: Raia wa Gaza wanakabiliwa na hali 'mbaya sana'
Zaidi ya Wapalestina 500 wameuawa huko Gaza kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel. Hilo ni jibu lililozoeleka huku maelfu ya wanajeshi wakitumwa kusini mwa Israel karibu na ukanda wa Gaza, ambako majeshi ya Israel yalijiondoa mnamo mwaka 2005. Lakini kitakachotokea baadaye ni vigumu mno kutabirika.
Sera ya kuwalinda mateka wote
Aaron David Miller, mtafiti mwandamizi katika shirika lilalochunguza masuala ya Amani ya Kimataifa "Carnegie" anasema ukweli ni kwamba kundi la Hamas limewachukua mateka watu hao kwa nia ya kujilinda dhidi ya hatua za kulipiza kisasi za Israel, haswa mashambulizi makubwa ya ardhini, lakini pia mateka hao wanawapa uwezo wa kulazimisha zoezi la kubadilishana wafungwa. David Miller anasema hilo litalazimisha jinsi Israel itakavyojibu hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya mateka.
Soma pia: Mzozo kati ya Israel na Hamas wazidi kutokota
Wizara ya mambo ya nje ya Israel imesema nchi hiyo itachukua hatua zitakazopelekea mateka wanaachiwa huru, na kwamba wataharibu vibaya miundombinu ya "magaidi wa Hamas" na kuhakikisha hakuna kundi lolote la kigaidi huko Gaza litakaloweza kuwadhuru tena raia wa Israel.
Lakini haitokuwa rahisi kwa Israel kuchukua maamuzi ili kufikia azma ya kufanikisha zoezi la kuachiwa huru mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas. Wakishambulia watasababisha pia vifo vya mateka hao, na wakifanya mazungumzo na Hamas ili kubadilishana wafungwa, itakuwa ni ushindi mkubwa kwa maadui hao wa Israel.
Chanzo:(RTRE)