Umoja wa Mataifa mbioni kutafuta makubaliano ya Dubai
11 Desemba 2023Akiwa anarejea tena Dubai baada ya mazungumzo ya usiku kucha ya wajumbe kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kufikia makubaliano kuhusu ulimwengu kuachana na uzalishaji wa mafuta ya visukuku.
Guterres aliwaambia wandishi habari kwamba wako mbioni ili kufikia makubaliano ya kihistoria.
"Mkutano wa Cop28 utahitimishwa kesho, lakini bado kuna mapungufu ambayo yanahitaji kuzibwa. Sasa ni wakati wa kuonyesha nia kubwa na kutafuta suluhisho. Mawaziri na wapatanishi lazima wajiepushe na hatua za kuharibu na mbinu zitakazozuia makubaliano. Ni wakati kujadili kwa nia njema na kushughulikia changamoto iliyowekwa na Rais wa COP Dk. Sultan Ahmed al-Jaber. Ni wakati wa kutafuta maelewano kwa ajili ya ufumbuzi, bila kuathiri sayansi au kuhatarisha haja ya kuwa na matarajio makubwa zaidi.", alisema Guterres.
Ukichochewa na maombi ya mataifa ya visiwa vidogo ambayo yanahofia kutoeka kwenye ramani, mkutano huo wa Dubai unazingatia wito wa kusitisha uzalishaji wa nishati ya visukuku, gesi na makaa ya mawe, yakiwa sababu kuu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Saudi Arabia, mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa mafuta duniani, imeongoza upinzani, huku kundi la nchi zinazozalisha mafuta duniani OPEC likiwataka wanachama wake kupiga kura ya kupinga kuondolewa kwa nishati ya visukuku.
Pingamizi la nchi wanachama wa OPEC
Bila kutaja nchi, Simon Stiell, mkuu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, alitoa wito kwa pande zote kuondoa vizuizi visivyo vya lazima vya kufikia makubaliano. Stiell alisema masuala mawili bado yanawagawanya wajumbe kwenye mkutano huo wa Dubai, ikiwa ni kuachana na nishati ya visukuku na kuharakisha ufadhili wa mabadiliko ya tabia nchi na mataifa tajiri kwa nchi zinazoendelea zilizoathirika zaidi.
Uongozi wa mkutano huo unatarajiwa kutoa rasimu mpya ya makubaliano hii leo Jumatatu. Mwenyekiti wa COP28 Sultan Al Jaber ametoa wito kwa nchi kukamilisha mambo kwa wakati ifikapo kesho Jumanne. Al Jaber, mkuu wa kampuni ya kitaifa ya mafuta ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ameahidi mara kwa mara kufikia makubaliano ya kihistoria na kuzitaka nchi kutafuta makubaliano na msingi wa pamoja juu ya nishati ya visukuku. Akisema Jumapili kwamba kushindwa kufikia makubaliano sio chaguo.
Msimamo wa China
Rasimu ya mwisho ya makubaliano iliyotolewa Ijumaa inajumuisha njia nne tofauti za kuondokana na nishati ya visukuku, lakini pia ina pendekezo la tano: kuacha suala hilo nje ya makubaliano ya mwisho.
China, nchi inayotoa gesi chafu zaidi duniani, pia ilionekana kupinga hatua ya kuachana na nishati ya visukuku lakini tangu wakati huo imekuwa ikifanya kazi kutafuta mwafaka.