UN: Hali katika Ukanda wa Gaza ni ya kutisha
13 Januari 2024Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kiutu nchini Israel na Palestina, Griffiths amesema kuwa katika karibu siku 100 za vita tangu Oktoba 7, watu 23,000 wameuwawa na 58,000 wamejeruhiwa. Ametoa takwimu hizo akiinukuu wizara ya afya ya Gaza na kuongeza kuwa asilimia 70 ya waliouwawa ni wanawake na watoto.
Soma zaidi: WHO yatoa wito wa kupunguza mateso ya watu wa Gaza
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa watu milioni 1.9 ambao ni asilimia 85 ya idadi jumla ya wakaazi wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi mfululizo yanayofanywa na Israel yakielekezwa kwa raia.
Ametanabaisha kwamba, hali ya mfumo wa afya inazidi kuzorota na kwamba huduma za kiutu zimekwama pakubwa ambapo wafanyakazi 148 wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wameuwawa. Pia Ofisi karibu 134 za Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA zimeshambuliwa.
Marekani yafanya mashambulizi mapya dhidi ya Wahouthi
Katika hatua nyingine, Marekani imefanya mashambulizi mapya dhidi ya waasi wa Houthi wa nchini Yemen na kulenga eneo linalozingatiwa kuwa tishio kwa meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, kwa mujibu wa maafisa wawili wa Marekani.
Maafisa hao walioomba wasitajwe majina, hawakutoa maelezo zaidi kuhusu mashambulizi hayo mapya. Mashambulizi hayo yamefanywa baada ya mengine 30 ya awali yaliyokuwa yamelenga kupunguza uwezo wa Wahouthi wa kuitishia njia ya kibiashara katika Bahari ya Shamu. Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, miundombinu iliyolengwa katika mashambulizi hayo ni pamoja na vituo vya kuhifadhi vifaa, mifumo ya anga na maghala ya silaha.
Soma zaidi: Guterres azionya pande husika kutozidisha mvutano Bahari ya Shamu
Hivi karibuni waasi wa Kihouthi walianzisha mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu ikiwa ni majibu kwa operesheni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la Hamas. Kundi hilo linatajwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.
Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa kiasi kikubwa wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen ukiwemo Mji Mkuu Sanaa.
Waasi hao wamezungumzia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi yao wakisema kuwa hayakusababisha majeruhi wala hasara ya mali
Naibu wa Mkuu wa shirika la habari la Wa Houthi Nasreddin Amer aliyasema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Jazeera ambapo aliongeza kuwa "Marekani itawajibika kwa uchokoz wake". Ameongeza kuwa watajibu mashambulizi hayo haraka iwezekanavyo.
Wanamgambo wa Kipalestina wauwawa Ukingo wa Magharibi
Jeshi la Israel limesema kuwa wanamgambo watatu wa Kipalestina wameuwawa wakati walipokuwa wakijaribu kuingia katika eneo la walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi mapema Jumamosi.
Kulingana na jeshi hilo, wavamizi walikuwa na visu, mashoka pamoja na bunduki. Mwanajeshi mmoja wa Israel alijeruhiwa katika tukio hilo.
Vurugu kwenye Ukingo wa Magharibi zimekuwa zikiongezeka tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.