Viongozi EU, UN walaani vurugu za Amsterdam
8 Novemba 2024Akizungumza na vyombo vya habari mjini Geneva msemaji wa Umoja wa Mataifa Jeremy Laurence ameeleza kuwa wameziona ripoti hizo zinazotia wasiwasi na kuwa hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa au kufanyiwa vurugu kwa misingi ya utaifa, dini, kabila au asili.
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X ameandika kuwa amekasirishwa na mashambulizi hayo mabaya dhidi ya Waisrael mjini Amsterdam.
Ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuzungumza na Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof na kuongeza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi barani Ulaya.
Waziri wa mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock ameelezea kushtushwa kwake na tukio hilo akisema kuwa ghasia za aina hiyo dhidi ya Wayahudi zinavuka mipaka yote na kuwa kitendo hicho ni aibu kwa Ulaya.
UEFA yaahidi kuchunguza vurugu za Amssterdam na kuchukua hatua stahiki
Nalo Shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA limelaani kile lilichokiita "matendo ya vurugu" yaliyotokea Alhamisi baada ya mechi kati ya Klabu za soka za Maccabi Tel Aviv na Ajax ya Uholanzi.
Kwa upande wake Meya wa mji mkuu wa Uholanzi Amsterdam Femke Halsema ameelezea kufedheheshwa kwake na tukio hilo na kusema kuwa, "Amsterdam inatazama nyuma katika usiku wa kutisha na bado hadi sasa ni kiza. Waandamanaji wenye chuki dhidi ya Wayahudi pamoja na wahalifu waliwashambulia na kuwapiga wageni wa Kiyahudi, Waisraeli katika mji wetu jana usiku. Natoa pole kwa waathiriwa na familia zao hapa na Israel."
Soma zaidi: Israel yatuma ndege mbili kuwaokoa raia wake Amsterdam
Mapema Ijumaa, polisi mjini Amsterdam kupitia jukwaa la X walichapisha taarifa kuwa, bendera ya Palestina ilishushwa kutoka mbele ya jengo moja na "watu wasiofahamika".
Baadaye ripoti zilidai kuwa mamia ya mashabiki wa Klabu ya Maccabi walikusanyika mbele ya uwanja wa Dam kuliporipotiwa kuwa na hali tete na kisha kukatulia.
Mamlaka za Uholanzi zimeripoti kuwa watu 62 wamekamatwa kutokana na vurugu hizo. Mamlaka ya viwanja vya ndege ya Israel imesema ndege ya kwanza iliyowabeba mashabiki hao kutoka Amsterdam imeshawasili katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion.