Ulaya yakabiliwa na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi
15 Novemba 2023Kwa miaka mingi, mataifa ya magharibi yamekuwa yakijaribu kuwalinda kwa hadhi maalum Wayahudi kutokana na historia yao. Wayahudi wamepitia madhila ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili, kutengwa na hata kuporwa mali zao.
Wakati wa vita vya pili vya dunia, utawala wa manazi wa Ujerumani ukiongozwa na Adolf Hitler uliendesha mauaji ya takriban wayahudi milioni 6. Mauji hayo ya kikatili huitwa pia Holocaust au Shoah. Si tu Ujerumani bali sehemu mbalimbali duniani walinyanyasika na mara kadhaa walilazimika kuwa wakimbizi.
Tangu kuibuka tena kwa mzozo huko Mashariki ya kati baada ya shambulio la kigaidi la kundi la Hamas kusini mwa Israel alfajiri ya Oktoba 7 na kusababisha vifo vya watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200, majibu ya Israel huko Gaza katika juhudi za kulitokomeza kundi hilo ambayo pia yamesababisha maelfu ya vifo, yameibua upya chuki dhidi ya wayahudi duniani kote hususan katika mataifa ya Magharibi.
Maandamano, kauli za chuki na vitisho, mauaji vimekuwa vikiripotiwa sehemu mbalimbali na hivyo kuzusha hofu miongoni mwa wayahudi ambao wamelazimika kuishi kwa kuficha imani yao.
Soma pia: Rais Emmanuel Macron awataka wafaransa wasimame kidete kupinga chuki dhidi ya Wayahudi nchini humo
"Ninapotoka nje huwa navaa kofia nyingine kuficha hii kofia ya kippah. Sasa hivi tumekuwa waangalifu mno tunapoingia na kutoka katika sinagogi au maduka yetu ya kosher," alisema Myahudi raia wa Ufaransa ambye hakutaka kutaja jina lake.
"Watu wengi wana wasiwasi kuhusu usalama wao. La kushangaza, mashambulizi na mauaji yamefanyika Israel, lakini watu wengi hapa bado wanahisi kuwa wako salama zaidi Israel kuliko hapa mjini Paris."
Ongezeko la matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi
Katika mwezi uliopita, mamlaka nchini Ufaransa imerekodi zaidi ya matukio 1,000 dhidi ya Wayahudi na kuwatia kizuizini karibu watu 486. Ufaransa imejibu vitendo hivyo kwa hatua kali na viongozi wa taifa hilo wameonyesha mshikamano na Israel na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya chuki dhidi ya wayahudi.
Sio hofu tu, Wayahudi waliopo katika mataifa ya magharibi wameanza pia kuchukua mikakati binafsi ya kujilinda mbali na hatua zinazochukuliwa na serikali za mataifa wanakoishi. Mfano nchini Marekani, baadhi ya wayahudi wameanza mafunzo ya kutumia silaha ili kujihami pale itakapohitajika.
Soma pia: Olaf Scholz aapa kufanya kazi na Israel kupeleka msaada Gaza
"Moyo wangu unaenda kasi sana na sitaki kabisa kuwa hapa. Lakini pia sitaki kuwa mtu ambaye, atashindwa kuchukua tahadhari sahihi au kujifunza kile kinachohitajika ili kuweza kujilinda na kuilinda familia yangu," alisema Corinne Feldmann, na Myahudi mama wa familia anayeishi huko Miami.
Viongozi Ufaransa washiriki maandamano ya kupinga chuko dhidi ya Wayahudi
Jumapili ya Novemba 12, kumefanyika maandamano makubwa nchini Ufaransa yaliojumuisha zaidi ya watu 180,000 ili kupinga kuongezeka kwa vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi. Wawakilishi wa vyama kadhaa vya mrengo wa kushoto, wahafidhina na wale wa mrengo wa kati wa Rais Emmanuel Macron pamoja na kiongozi wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen walihudhuria maandamano hayo.
" Idadi kubwa mno ya wananchi wamekusanyika kuitikia wito uliyotolewa na maspika wa baraza la Seneti na Bunge. Ni wazi kwamba ilikuwa muhimu kwangu kujumuika pamoja na serikali kusema kwamba ni lazima Ufaransa iwalinde raia wake wote ambao wanaweza kuwa na wasiwasi kwa sababu ya asili au dini yao. Pamoja na serikali na mawaziri wote, tunataka kuwaambia wananchi wenzetu wa imani ya Kiyahudi kwamba tuko upande wao. Tumehamasika na kamwe hatutaruhusu uhalifu wowote," alisema Waziri Mkuu wa Ufaransa, Elisabeth Borne kufuatia maandamano hayo.
Soma pia:Bunge la Ufaransa kupiga kura ''kuitambua'' Palestina
" Kuna bendera nyingi za Ufaransa katika maandamano haya, lakini kinachotuunganisha sio bendera tu, ni kile kinachowakilishwa na bendera hiyo. Yaani thamani ya uhuru na thamani ya utu wa binadamu. Kwa maana hiyo chuki dhidi ya Wayahudi ni shambulio dhidi ya misingi ya bendera hiyo na shambulio dhidi ya nchi hii," aliongeza Rais wa zamani wa taifa hilo, Francois Hollande.
Chuki dhidi ya Wayahudi na hatari ya kupoteza haki ya ukazi Ujerumani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na hata yule wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir tayari wamefanya mikutano tofauti na kuzungumza na viongozi wa dini mbalimbali katika mataifa yao ili kukabiliana na vitendo vinavyoongezeka vya chuki dhidi ya wayahudi. Lakini Kansela Olaf Scholz amesisitiza kuwa hilo kamwe halikubaliki nchini Ujerumani.
"Hakuna kitu chochote, iwe asili ya mtu, misimamo ya kisiasa, tamaduni au hata historia ya baada ya ukoloni vinavyoweza kumpa mtu uhalali wa kusherehekea mauaji, mauaji ya kikatili ya watu wasio na hatia. Na kwa hakika, kila mtu anahitaji kufahamu kwamba chuki dhidi ya wayahudi inakuweka pia katika hatari ya kupoteza kibali cha mkazi hapa Ujerumani," alisitiza Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.
Wakati viongozi wa nchi za Magharibi wakionesha mshikamano kwa Israel katika vita vyake na Hamas huko Gaza, hali imekuwa tofauti kwa vijana wengi ambao wanaoonekana kukosoa vitendo vya Israel huko Gaza na kuiunga mkono Palestina katika azma yao ya kuunda taifa lao lililo huru na kukomesha ukaliaji wa israel.
Rais wa sasa wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitiza umuhimu wa kutokuwa na undumilakuwili. Ametoa wito wa kuhakikisha wakazi wa Gaza wanalindwa na haki yao ya kukaa ardhi yao inalindwa.
Soma pia: Scholz ahimiza ujasiri wa kiraia kuwalinda Wayahudi
"Leo hii raia wa Gaza wanateseka. Takriban watu milioni moja na nusu wameyakimbia makazi yao na maelfu wamekufa au kujeruhiwa. Waisrael na Wapalestina wote wamepitia masaibu. Hatuwezi kuafiki hili, kwa sababu maisha ya kila mmoja yana thamani iliyo sawa," alisema Macron katika mahojiano na shirika la Utangazaji la Uingereza BBC.
"Kwa sisi watetezi wa maadili ya ubinaadamu, hatuwezi kuwa na undumilakuwili. Ni lazima tujifunze kutokana na makosa yetu na tusikubali tena suala la amani katika Mashariki ya Kati kuwa linaahirishwa kila mara. Lazima tuchukue hatua kuelekea suluhu ya mataifa mawili yaliyo huru, Israel na Palestina zikiishi kama majirani kwa amani na usalama."