Umoja wa Ulaya kuichukulia hatua kali Niger
18 Agosti 2023Kamishna wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, Abdel Fatau Musah, alisema matumizi ya nguvu bado yanasalia kuwa hatua ya mwisho watakayochukua. Musah aliendelea kusema kuwa majeshi ya jumuiya hiyo yako tayari iwapo juhudi zote zingine hazitozaa matunda.
Afisa huyo anayehusika na masuala ya siasa na usalama wa Jumuiya ya ECOWAS amesema sehemu kubwa ya wanachama wa ECOWAS wako tayari kutoa wanajeshi washiriki uvamizi huo isipokuwa nchi tatu zilizo chini ya tawala za kijeshi, Mali, Burkina Faso, na Guinea - pia taifa la Cape Verde.
Hata hivyo wataalamu wa masuala ya kiusalama wamesema hatua yoyote ya kijeshi itakayochukuliwa italiyumbisha eneo zima la Sahel ambalo limekuwa likipambana na mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu kwa kipindi cha mwongo mmoja sasa.
Vitisho vya hatua kali vya jamii ya kimataifa
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel alionya kuwepo na hatua kali ikiwa utawala wa kijeshi wa Niger utasababisha afya ya Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kuzorota zaidi chini ya kifungo cha nyumbani.
Katika mazungumzo ya simu na Rais Bola Tinubu wa Nigeria, ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya kikanda ya ECOWAS, Charles Michel alisema hali ya kuwekwa kizuizini kwa Rais Bazoum inazidi kuzorota.
''Kuhakikisha mustakabali wa bara letu''
Huko Niger kwenyewe, Boubacar Sabo, Katibu Mkuu wa chama tawala cha PNDS nchini humo, anasema endapo mapinduzi ya Niger yatafanikiwa basi utakuwa ni mwisho wa demokrasia barani Afrika.
"Rais wa Jamhuri, Mohammed Bazoum ametekwa nyara na kuzuiliwa tangu Julai 26 na walinzi wake. Tunaamini kuwa kinachoendelea Niger ni ujumbe sio tu kwa eneo la Sahel, hii inatia shaka utaratibu wa kidemokrasia katika nchi za Afrika Magharibi na Afrika kwa ujumla. Ikiwa tutapigana leo ni kuzuia mambo ya aina hii kutokea na kuhakikisha mustakabali wa bara letu.", alisema Sabo.
Uhuru na demokrasia hatarini
Kwa upande wake, Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk amesema hakuna msingi wa kisheria kwa jeshi la Niger kumfungulia mashitaka ya uhaini rais Mohamed Bazoum. Turk amesema hatua hiyo imeweka hatarini uhuru na demokrasia, na uamuzi huo sio tu wa kisiasa dhidi ya Rais aliyechaguliwa kidemokrasia lakini hauna msingi wa kisheria. Volker Turk amesema utawala wa mtutu wa bunduki hauna nafasi katika ulimwengu wa sasa.
Mpaka sasa, inaripotiwa kuwa kuna mgawanyiko kati ya nchi wanachama iwapo jeshi litumwe nchini Niger. Hata hivyo, Maseneta nchini Nigeria, ambayo ndio Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya ECOWAS, wamepinga mpango wa jeshi la nchi yao kwenda Niger.