1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa majeshi ya ECOWAS kuhitimisha mipango kuhusu Niger

18 Agosti 2023

Wakuu wa majeshi wa mataifa ya Afrika Magharibi watafanya mkutano kwa siku ya pili na ya mwisho leo katika mji mkuu wa Ghana, Accra. Mkutano huo unajadili uwezekano wa kuivamia Niger kurejesha uongozi wa kikatiba.

https://p.dw.com/p/4VJXe
Wakuu wa majeshi ya nchi katika jumuiya ya ECOWAS wakikutana Accra Ghana Agosti 17, 2023
Wakuu wa majeshi ya nchi katika jumuiya ya ECOWAS wakikutana Accra Ghana Agosti 17, 2023Picha: Richard Eshun Nanaresh/AP/dpa/picture alliance

Wakuu hao wamekuwa wakijadili uwezekano wa kufanya uvamizi wa dhidi ya Niger, iwapo juhudi za kidiplomasia zitagonga mwamba.

Kamishna wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, Abdel Fatau Musah, alisema mwanzoni mwa mkutano huo siku ya Alhamisi kwamba, matumizi ya nguvu bado yanasalia kuwa hatua ya mwisho watakayochukua ila akasema majeshi ya jumuiya hiyo yako tayari iwapo juhudi zote zingine hazitozaa matunda.

Musah amesema sehemu kubwa ya wanachama wa ECOWAS wako tayari kutoa wanajeshi washiriki uvamizi huo isipokuwa nchi tatu zilizo chini ya tawala za kijeshi - Mali, Burkina Faso, Guinea - pia taifa la Cape Verde.

Hatua yoyote ya kijeshi itakayochukuliwa italiyumbisha eneo zima la Sahel ambalo limekuwa likipambana na mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu kwa kipindi cha mwongo mmoja sasa.