1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yajadili mzozo wa Idlib

6 Machi 2020

Mataifa ya Umoja wa Ulaya yameyakaribisha makubaliano ya Uturuki na Urusi kuhusu kusitisha mashambulizi nchini Syria, lakini kwa tahadhari kubwa na kuomba pande zinazotifautiana kuruhusu misaada ya kiutu.

https://p.dw.com/p/3YyxG
Kroatien Treffen EU-Außenminister in Zagreb Josep Borrell
Picha: Getty Images/AFP/D. Sencar

Huku kukitolewa mwito huo, kumeripotiwa mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Syria na waasi mkoani Idlib yaliyosababisha vifo vya wanajeshi 15 wa serikali na washirika wake. 

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya wanakutana katika mji wa Zagreb, Croatia kwa mazungumzo kuhusu mzozo katika mkoa wa Idlib kaskazinimagharibi mwa Syria, ambako Ankara na Moscow zinasaidia pande tofauti zinazopambana kwenye mzozo huo.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo, yanalenga kusitisha mapigano makubwa yaliyochochea kusambaa kwa mzozo wa kiutu.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Ulaya Josep Borrel amenukuliwa akisema ameridhishwa na makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano na ni habari njema na anachosubiri kuona ni namna yatakavyofanya kazi, huku akiyatolea mwito mataifa ya Ulaya kuhakikisha wanapata majibu ya namna yatakavyoendeleza ushirikiano na Uturuki na Urusi, ambao kwa muda mrefu umekuwa tete.

"Kesho itakuwa ni siku rasmi ambapo tutakubaliana azimio kuhusu eneo la mashariki mwa Mediterania, na Uturuki na Urusi zimekuwa kwenye ajenda yetu. Mahusiano yetu na mataifa yana mawili yamekuwa magumu kwa kweli, lakini tunalazimika kuyaboresha kwa kuzingatia mitizamo mbalimbali. Tunalazimika kuanza na mbinu mpya ili kukabiliana na ugumu huu.", amesema Borrel.

Kroatien Treffen EU-Außenminister in Zagreb
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wakiwa mjini Zagreb, ambapo miongoni mwa masuala muhimu ni mahusiano yao na Urusi na UturukiPicha: Imago Images/photothek/J. Schmitz

Mawaziri hao aidha wametoa mwito wa uwezekano wa masharti makali zaidi, ili mpango huo wa kusitisha mapigano uweze kutekelezeka pamoja na kuwalinda raia na kuondoa vizingiti vya uingizwaji wa misaada ya kiutu kutoka kwa jamii ya kimataifa. Umoja wa Ulaya umetangaza msaada wa euro milioni 60 kwa ajili ya eneo hilo la kaskazinimagharibi mwa Syria, ambayo ni sehemu ya euro milioni 170 kwa ajili ya wahitaji kote nchini Syria.

Borrel awaambia wahamiaji "mipaka haijafunguliwa".

Baadhi ya mataifa ya Ulaya na hususan Uholanzi wametaka marufuku ya kuruka ndege kwenye anga ya Idlib ili kuzuia mashambulizi ya angani yanayofanywa na serikali. Lakini maafisa hao hawana uwezo wa kutekeleza hayo, na wanatilia shaka.

Huku wakijadili hayo, shirika la kusimamia haki za binaadamu la Syria lenye makao yake Uingereza, limesema kumekuwepo na mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali katika mji wa Jabal al-Zawiya, mkoani Idlib na kusababisha vifo vya wanajeshi 15 wa serikali na washirika wao. Mapigano hayo yalitokea masaa matatu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, lakini tangu hapo kumekuwa na utulivu, limesema shirika hilo.

Na huko kwenye mpaka wa Ugiriki na Uturuki kumezuka mapigano kati ya maelfu ya wahamiaji wanaoshinikiza kuvuka na kuingia Ulaya na vikosi vya kulinda mipaka. Polisi ya Ugiriki ilirusha mabomu ya kutoa machozi kwa wahamiaji waliojaribu kuvunja uzio, ambao pia walijibu kwa kuwarushia mawe, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la AFP.

Mkuu wa sera za kigeni za Ulaya, Borrel akiwa Croatia amewaambia wahamiaji hao kwamba "mipaka na Uturuki haijafunguliwa" na kuwataka waandishi wa habari kuwafikishia ujumbe huo.

Mashirika: DPAE/AFPE/APE