Mashambulizi ya serikali ya Syria yasababisha vifo 20 Idlib
26 Februari 2020Shirika la Kusimamia Haki za Binadamu nchini Syria limesema miongoni mwa watu hao waliouwa, tisa ni watoto. Vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi vinaendeleza kampeni kapambe ya mashambulizi katika mkoa wa Idlib ambao ni wa mwisho nchini humo unaodhibitiwa na waasi pamoja na wanajihadi.
Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema mashambulizi ya mji wa Idlib wenye jina sawa na mkoa huo, yamesababisha kifo cha wanafunzi mmoja na walimu watatu. Wanafunzi wengine sita ni miongoni mwa watu 10 waliouawa katika mji wa Maarat Misrin, ulio kaskazini mwa mji wa Idlib. Abdel Rahman ameongeza kwamba watoto wengine wanne, ikiwa ni pamoja na mama mmoja na watoto wake wawili, wameuawa katika mashambulizi ya serikali katika mji wa Binnish kaskazini-mashariki mwa Idlib.
"Nilikuwa nafungua mlango wa duka kutaka kuingia ndani, na vijana walikuwa wanatoa bidhaa nje, tulikuwa tukifagia na kusafisha dukamara ghafla tulisikia kitu kizito kinatuangukia kutoka juu, hatukujua kinachoendelea. Duka limeharibika, na sisi tumejeruhiwa vibaya. Kwanini wanatulenga sisi, tuna kipi cha maana?" analalamika muuza duka katika mkoa wa Idlib, Abdul Hakim Qassas.
Baadae kidogo shirika hilo la kusimamia haki za binadamu limeripoti kwamba vikosi vya serikali vimefanikiwa kukamata miji 19 na vijiji vingine kadhaa katika kipindi cha masaa 48.
Soma zaidi:Umoja wa Ulaya waitaka Syria kusitisha mashambulizi Idlib
Waasi warejesha udhibiti mji wa Nairab, Idlib
Kwengineko katika mkoa huo wa Idlib, waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki nao wametangaza kuukamata mji wa Nairab. Maafisa wa vikosi vya Uturuki pamoja na waasi wamesema jana kwamba huo ni mji wa kwanza waliofanikiwa kurejesha udhibiti baada ya kuvipokonya vikosi vya serikali.
Vurugu hizo zimefanyika huku Rais wa Uturuki akitangaza kwamba ujumbe wa Urusi utawasili siku ya pili kuanzisha tena mazungumzo yenye lengo la kupunguza mivutano katika mkoa huo wa Idlib.
Urusi imetangaza jana kwamba haitokubaliana na makundi ya waasi inayoyazingatia kuwa ni ya kigaidi kusitisha mapigano katika mkoa wa Syria wa Idlib. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov amesema mapatano yatawahamasisha waasi kuendelea kukiuka sheria za kimataifa.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imezitolea wito pande zinazopigana kuruhusu njia salama ya raia wa kawaida kukimbia mashambulizi hayo. Vurugu za mkoa wa Idlib zimesababisha idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao katika historia ya dunia ya miaka ya hivi karbuni pamoja na idadi kubwa ya vifo.
Vyanzo: (afp, rtre)