1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kushinikiza mashitaka dhidi ya Lukashenko

6 Oktoba 2021

Bunge la Ulaya limeonyesha utayari wa kuishinikiza zaidi jumuiya ya kimataifa kumshitaki rais wa Belarus Alexander Lukashenko anayehusishwa na ukandamizaji na mateso ya watu wengi.

https://p.dw.com/p/41KRU
Belarus Präsident Alexander Lukaschenko
Picha: Maxim Guchek/BelTA Pool Photo via AP/picture alliance

Wabunge wa bunge la Ulaya wanakutana mjini Strasbourg nchini Ufaransa huku wakionyesha utayari wa kuishinikiza zaidi jumuiya ya kimataifa kumshitaki rais wa Belarus Alexander Lukashenko anayehusishwa na ukandamizaji na mateso ya watu wengi.

Wabunge hao wamesema rais Lukashenko kinyume cha sheria aliagiza kukamatawa na kuteswa wafuasi wa upinzani waliopinga matokeo yaliyozozaniwa ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 2020. Takriban watu 700 waliokamatwa, bado wanazuiwa vizuizini.

Jana Jumanne, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Lithuania na mbunge wa bunge hilo Andrius Kubilius aliliambia bunge mjini Strasbourg kwamba Lukashenko anatakiwa kufikishwa kwenye mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, matamshi yaliyoungwa mkono na mbunge kutoka Ujerumani Sergey Lagodinsky, aliyesema hatua hizo za kisheria zinatakiwa kuanzia kwa Lukashenko mwenyewe.

Soma Zaidi: Lukashenko azishutumu nchi za Magharibi kuanzisha vita dhidi yake

Mjadala huo wa Strasbourg pia uliangazia masuala ya wahamiaji na hususan kutokea nchini Iraq ambao Minsk inawahamishia kwenye maeneo ya mipaka baina yake na Poland, Lithuania na Latvia. Mataifa hayo matatu yanasalia katika hali ya dharura baada ya zaidi ya wahamiaji 6,000 kuvuka mpaka kinyume cha sheria kwa mwaka huu, idadi ya juu ikilinganishwa na 150 waliovuka mwaka uliopita.

Jumla ya maafisa 166 wa juu wa Belarus wanakabiliwa na hatua ya kuzuiwa mali zao na zuio la kusafiri. Lakini pia tayari Umoja huo umeiwekea Belarus vikwazo vya kiuchumi. 

EU-Westbalkan-Gipfel in Slowenien | Ursula von der Leyen
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema wanalazimika kuyachukulia mataifa ya Balkani kama familia ya UlayaPicha: Petr David Josek/dpa/AP/picture alliance

Ulaya yahamasisha kuyakubali mataifa ya Balkani.

Huku hayo yakiendelea, huko nchini Slovenia, rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema hii leo kwamba viongozi wa muungano huo wanatakiwa kupeleka ujumbe chanya kwenye mataifa sita ya Balkani yenye nia ya kujiunga na umoja huo, licha ya kuzorota kwa majadiliano.

Soma Zaidi: Albania na Macedonia zasubiri ridhaa kuingia Umoja wa Ulaya

Amesema, wanataka kutuma ujumbe ulio wazi kwa mataifa hayo kwamba, wao pia ni miongoni mwa familia ya Ulaya, matamshi yake yanayoungwa mkono na kansela wa Austria Sebastian Kurz.

"Eneo la Balkani ya Magharibi liko karibu sana na sisi. Sio tu kihistoria, bali pia kijiografia na haswa kiuchumi na kibinadamu. Na ninaamini ikiwa sisi kama Umoja wa Ulaya hatutakuwa na mtizamo thabiti juu ya eneo hili, basi ni lazima tujue kuwa madola mengine makubwa kama China, Urusi au hata Uturuki wanaongeza ushawishi wao huko. Kanda hii iko Ulaya kijiografia na inahitaji pia mtazamo wa Ulaya. ", alisema Kurz.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wako mjini Kranj, Slovenia kwa ajili ya mkutano wa kilele wa umoja huo kuhusiana na masuala ya Balkani ya Magharibi, ambao pamoja na mjadala kuhusiana na eneo hilo, masuala kuhusu Afghanistan, COVID-19 na matokeo ya uchaguzi wa shirikisho la Ujerumani yanatarajiwa kupewa kipaumbele.

Mashirika: RTRE/DW