Ukraine: Urusi ilitumia makombora iliyopewa na Pyongyang
5 Januari 2024Kauli ya Kyiv inathibitisha tamko la Marekani lililoishutumu Moscow kuwa ilitumia silaha zilizotolewa na Pyongyang katika mashambulizi yake ya hivi karibuni nchini Ukraine.
Tamko hilo limetolewa na Mshauri wa Rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak baada ya hapo awali Kyiv kusema kuwa haikuweza kuthibithisha iwapo Urusi ilitumia makombora iliyopewa na Korea Kaskazini. Hata hivyo Podolyak hakutoa ushahidi wowote iwapo makombora yaliyotumiwa na Urusi katika mashambulizi ya hivi majuzi nchini Ukraine yalitolewa na Korea Kaskazini.
Soma pia: Pyongyang yakosoa matamshi ya Blinken juu ya uhusiano wake na Urusi
Licha ya kuwa Marekani haikuweka wazi ni aina gani ya makombora ambayo Pyongyang inaweza kuwa iliipatia Urusi, msemaji wa Ikulu ya Marekani John Kirby amesema makombora hayo yana uwezo wa kusafiri hadi kilometa 900 kutoka sehemu yalikofyetuliwa. Moscow na Pyongyang wamekuwa wakikanusha mara kadhaa kusaini mikataba yoyote ya silaha.
Korea Kaskazini imekuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya silaha tangu ilipofanya jaribio la bomu la nyuklia mnamo mwaka 2006.Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yaliidhinishwa pia na Urusi, yanazipiga marufuku nchi zote kufanya biashara ya silaha au vifaa vya kijeshi na Korea Kaskazini.
Soma pia: Ikulu ya White House imesema kwamba Urusi ilitumia makombora ya Korea Kaskazini dhidi ya Ukraine
Hayo yanajiri wakati mapambano makali yameendelea kushuhudiwa. Ukraine imesema usiku wa kuamkia leo, wameshambuliwa na takriban droni 30 za Urusi zilizotengenezwa na Iran za "Shahed" lakini wamefanikiwa kudungua droni 21 kati ya hizo. Kwa upande wake pia Moscow imesema imefanikiwa kudungua droni kadhaa za Ukraine katika mji wa Belgorod na katika rasi ya Crimea.
Kufuatia mashambulizi makubwa ya Ukraine katika mji huo wa mpakani wa Belgorod, Moscow imetangaza hii leo kuwa tayari kuwahamisha baadhi ya wakazi kutoka mji huo.
Kundi la mataifa ya G7 kuendelea kuisaidia Ukraine
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni ameihakikishia Ukraine uungwaji mkono usioyumba wa kundi la mataifa saba tajiri na yaliyostawi kiviwanda ya G7.
Zelensky amemshukuru Meloni kwa msaada wake, ikiwa ni pamoja na kupiga jeki nia ya Ukraine ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo rais huyo wa Ukraine amesema ana matumaini ya kupata msaada zaidi wa kijeshi ili kujilinda.
"Walinzi wetu wa anga wanafanya kila waliwezalo kuilinda nchi. Timu nzima ya wanadiplomasia wetu, wale wote wanaohusika na mawasiliano na washirika wetu pamoja na wawakilishi wa Ukraine kimataifa, wanafanya kila wawezalo ili kuhakikisha tunapata mifumo zaidi ya ulinzi wa anga na makombora. Hiki ndicho kipaumbele nambari moja."
Kulingana na vyombo vya habari vya Italia, Meloni alizungumza kwa njia ya simu na rais Volodymyr Zelensky na alieleza kuwa vita vya uchokozi vya Urusi dhidi ya jirani yake, itakuwa mada itakayopewa kipaumbele katika awamu ya Urais wa kupokezana wa kundi la G7 ambao sasa unashikiliwa na Italia tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2024. Wanachama wa G7 ni Marekani, Ujerumani, Canada, Uingereza, Japan, Italia na Ufaransa.