1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya msimamo: Ujerumani kuiuzia silaha Saudi Arabia

12 Januari 2024

Serikali ya Ujerumani imebadili msimamo wake kuhusu uuzaji wa silaha nje ya nchi.Inataka kuruhusu upelekaji wa makombora chapa IRIS-T kwa ndege za kivita za Eurofighter nchini Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/4bANy
Ujerumani| Kansela wa Shirikisho Olaf Scholz akitembelea kikosi cha naga mjini Jagel
Serikali ya Ujerumani inaruhusu uuzaji wa silaha kwa Saudi ArabiaPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ilikuwa ni serikali ya kihafidhina inayoongozwa na Kansela Angela Merkel ambayo ilizuia silaha za Ujerumani kuuzwa Saudi Arabia mwezi Oktoba mwaka 2018. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, na Saudi Arabia kuhusika kwenye vita vya Yemen, ambako muungano wa kijeshi wa mataifa ya Kiarabu unapambana dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, chini ya uongozi wa Saudia. Vita hivyo vimesababisha mojawapo ya mizozo mibaya zaidi ya kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni.

Sasa, miaka mitano tu baadae, serikali inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz inatathmini upya uhusiano wake na serikali ya Saudia. Wakati wa ziara yake mjini Jerusalem Januari 7, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alisema kufuatia shambulizi la kigaidi lililofanywa na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, Saudi Arabia imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa usalama wa Israel. Baerbock kutoka chama cha Kijani, amesema hatua hiyo insaidia kuzuia hatari ya mzozo kuenea katika ukanda huo.

Saudi Arabia | Eurofighter Typhoon
Ndege za Eurofighter za jeshi la anga la Saudi Arabia katika anga ya RiyadhPicha: Fayez Nureldine/AFP/Getty Images

Muungano unaotawala wa chama cha Social Democratic SPD, chama cha Kijani na kile cha waliberali FDP, umetafakari upya. Mwishoni mwa mwezi Desemba, serikali ya Ujerumani ilisema imeidhinisha kuuza makombora 150 chapa IRIS-T kwenda Saudi Arabia. Januari 10, msemaji wa serikali, Steffen Hebestreit alithibitisha kuhusu hilo.

Soma pia: Mauzo ya nje ya silaha ya Ujerumani yaongezeka

Waziri wa mambo ya nje pia hataki tena kuzuia uuzaji wa ndege za kivita za Ulaya kwenda Saudi Arabia. Tayari kuna ndege za kivita 72 chapa Eurofighter zinazoendeshwa zikiwa na bendera ya familia ya kifalme ya Saudia. Uingereza ingependa kupeleka ndege 48 zaidi. Lakini hilo litahitaji idhini ya serikali ya Ujerumani, kwa sababu ndege za Eurofighter, ambazo pia zinajulikana kama Typhoon ni mradi wa ushirikiano wa pamoja wa nchi hizo.

Tofauti katika makubaliano ya muungano

Kundi kubwa zaidi la upinzani kwenye bunge la Shirikisho la Ujerumani, Bundestag, kambi ya vyama vya muungano wa kihafidhina vya CDU na CSU, umepongeza hatua hiyo ya serikali ya shirikisho. Hata hivyo, kuna upinzani ndni y serikali yenyewe, kutoka kwa wabunge wa chama cha Kijani, ambao walishangazwa na tangazo la Waziri Baerbock.

Soma pia: Biden kusitisha mauzo ya silaha UAE na Saudi Arabia

Sara Nanni, msemaji wa sera ya ulinzi wa kundi la wabunge wa chama cha Kijani katika bunge, amesema kuwa suala la kuuza silaha siku zote limekuwa la msingi kwa chama wa Kijani. Nanni ameiambia DW kuwa makubaliano ya muungano kati ya vyama vya SPD, FDP na Kijani tangu mwaka 2021 yanasema wazi kwamba hakutakuwa na idhini ya kuuza silaha kwa nchi yoyote ambayo inahusika moja kwa moja katika vita nchini Yemen.

Kwa mujibu wa Nanni, chama cha Kijani kilikubali silaha kupelekw Ukraine, kutokana na sababu nzuri za kuipa demokrasia ambayo imevamiwa kwa mara ya pili na Urusi, kwa lengo la kujilinda na kujitetea. Amebainisha kuwa haoni sababu yoyote nzuri linapokuja suala la Saudi Arabia. Saudia inachukuliwa kama soko kubwa la vifaa vya kijeshi. Nchi hiyo ambayo mara kwa mara iko katika orodha ya chini kwenye utafiti wa haki za binadamu na demokrasia, ilitumia takribani euro bilioni 68.5 kwa ajili ya silaha mwaka 2022 pekee.

Soma pia: Ujerumani kutafakari udhibiti wa silaha

Hatua ya serikali ya Ujerumani kubadili mtazamo wake, sasa inapaswa kuongeza matumaini ya kupata mikataba mipya ya mabilioni ya euro. Matthias Wachter, kutoka chama cha viwanda, BDI amesema hatua ya Ujerumani kubadili msimamo wake wa kuiuzia Saudia silaha ni wa haki na muhimu.

Wachter ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa uamuzi huo utaisaidia Israel na kuizuia Ujerumani kutengwa barani Ulaya katika muktadha wa sera ya silaha. Anasema ushirikiano zaidi wa Ulaya katika sera ya usalama, unawezekana tu kwa kuaminiana, na sio kwa njia ya kura ya turufu.