Ujerumani yauza silaha za €1 bilioni Mashariki ya Kati
3 Januari 2021Kwa mujibu wa duru za wizara ya uchumi ya Ujerumani, silaha hizo ziliuzwa mwaka uliopita, 2020 kwa jumla ya euro bilioni 1.16. Hadi kufikia Desemba 17, 2020, Ujerumani ilisaini ruhusa ya kuuza silaha na vifaa vya kijeshi vyenye thamani ya euro milioni 752 nchini Misri.
Idhini hiyo pia ilitolewa kwenye kampuni za silaha za Ujerumani kwa mikataba yenye thamani ya zaidi ya euro milioni 305.1 kwa Qatar, zaidi ya euro milioni 51 kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, euro milioni 23.4 kwa Kuwait na takriban euro milioni 22.9 kwa Uturuki. Vibali vilivytolewa kwa Jordan ni jumla ya euro milioni 1.7 na Bahrain jumla ya euro milioni 1.5.
Soma zaidi: Uuzaji wa silaha duniani waongezeka kwa 8%
Mchanganuo huo umetolewa na wizara ya uchumi ikiwa ni katika kujibu swali la mbunge wa Chama cha Kijani, Omid Nouripour ambayo imenukuliwa na shirika la habari la Ujerumani, DPA.
Uhusiano na Yemen, Libya
Nchi zilizotajwa zote zinahusika katika mizozo ya Yemen na Libya. Nchini Yemen, tangu mwishoni mwa mwaka 2014 muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukiiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran. Muungano huo unazijumuisha Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Kuwait, Jordan na Bahrain.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kiutu inakadiria kuwa watu 233,000 walikufa kutokana na vita vya Yemen vilivyodumu kwa miaka sita. idadi hiyo inawajumuisha watu 131,000 waliouawa kutokana na visa visivyo vya moja kwa moja kama vile kukosa chakula, huduma za afya na miundombinu.
Wakati huo huo, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya vimekuwa vikiendelea tangu mwaka 2014 na maelfu wameuawa. Qatar na Uturuki zinaiingilia katika upande wa serikali inayotambuliwa kimataifa ya GNA inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj mjini Tripoli.
Kwa upande mwingine, mbabe wa kivita Khalifa Haftar anaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri. Kwa hivi sasa kuna makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Libya, hatua inayoleta matumaini ya kumalizika kwa vita na amani kupatikana.
Wakati huo huo, Ujerumani inashiriki katika juhudi za kuleta suluhisho la mgogoro wa nchini Libya na inafanya juhudi ili kuzuia silaha kupelekwa nchini humo.
Ujerumani miongoni mwa wauzaji wa juu wa silaha
Ujerumani ni miongoni mwa nchi tano za juu duniani zinazouza silaha nchi za nje, ikiwa pamoja na Marekani, Urusi, Ufaransa na China. Hii ni kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti kuhusu Amani, SIPRI.
Ripoti ya SIPRI inaeleza kuwa kwa pamoja nchi hizo zilijumuisha asilimia 76 ya mauzo yote ya silaha mnamo mwaka 2015 hadi 2019.
(DPA, DW https://bit.ly/38TDPFa)