Mauzo ya nje ya silaha ya Ujerumani yaongezeka
24 Januari 2018Serikali hiyo ya muungano imeidhinisha mauzo mengi ya silaha katika muda wa miaka minne, na kuzusha mjadala juu ya sera ya nchi hiyo ya mauzo ya silaha.
Serikali ya kansela Angela Merkel imeidhinisha zaidi ya mauzo ya silaha yenye thamani ya euro bilioni 25.1 sawa na dola za Kimarekani bilioni 30.9 tangu kuingia madarakani mwaka 2014.
Hii inaifanya serikali ya sasa , muungano kati ya chama cha kansela Merkel cha Christian Democratic, CDU na kile cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha SPD , kuwa imefanya mauzo zaidi kuliko serikali yoyote ya Ujerumani katika enzi za sasa, kituo cha televisheni cha taifa ARD kimeripoti.
Mabadiliko muhimu yamekuja katika mauzo kuelekea katika mataifa nje ya Umoja wa Ulaya na NATO , serikali ya mjini Berlin iliidhinisha mauzo ya silaha yenye thamani ya euro bilioni 14.48 kati ya mwaka 2014 na 2017. Hii ni ongezeko la asilimia 47 ikilinganishwa na baraza la mawaziri la mwaka 2010-2013.
Kabla ya makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya mseto mwaka 2013, chama cha SPD kiliahidi kuweka sheria kali katika mauzo ya silaha. Makubaliano hayo pia yalisababisha kuwekwa Sigmar Gabriel wa SPD kuwa mkuu wa wizara ya uchumi , na kumpa nafasi ya kuangalia mauzo.
Mauzo ya nje ni makubwa
Kituo cha televisheni cha ARD cha Ujerumani kimesema ripoti yake imo katika misingi ya data zilizotolewa na wizara ya uchumi, kufuatia uchunguzi uliofanywa na chama cha Die Linke.
Kituo hicho cha televisheni kimesema data hizo ni za awali na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka.
"Miaka minne iliyopita, SPD iliahidi kujiweka mbali na sera ya mauzo ya nje ambayo yatakuwa katika msingi wa uchumi," Stefan Liebich kutoka chama cha Die Linke alikiambia kituo cha ARD.
"Katika hali ya kawaida, milango haikufungwa , lakini ilifunguliwa wazi zaidi."
Kiongozi huyo wa wabunge wa chama cha Die Linke Dietmar Bartsch alikwenda umbali zaidi leo (jana), kwa kusema ni vigumu kuamini kwamba Ujerumani itapeleka silaha kwa mataifa yanayoongozwa na madikteta.
"Tarakimu ambazo zimechapishwa hivi sasa zinaonesha kwamba kuna hatua pia kuporomoka kwa uadilifu ambao sijawahi kufikiria kuwa unawezekana," Bartsch alisema, akielezea mauzo hayo kuwa ni "kushindwa kwa jumla" kwa serikali ya muungano.
Mwanasiasa huyo wa siasa za mrengo wa kushoto alisema usafirishaji wa silaha kutoka Ujerumani kwenda Uturuki kunahitajika kusitishwa mara moja."
Chama cha Kijani cha Ujerumani pia kimeikosoa vikali serikali , kikisema kushindwa kwao kuzuwia mauzo ya nje ya silaha ni ishara ya kuwa "muflisi".
Sheria za mauzo
Baraza la mawaziri limekuwa likikiuka sheria zake wenyewe katika mauzo ya nje ya silaha, alisema mtaalamu wa chama hicho wa masuala ya sera za nje Omid Nouripour, licha ya mahubiri aliyotoa kwa Sigmar Gabriel.
Mnunuzi mkubwa wa silaha za Ujerumani ni Algeria , ambayo imenunua kiasi cha silaha zenye thamani ya euro bilioni 1.36 katika miaka ya hivi karibuni.
Orodha ya mataifa kumi ina mataifa matatu ya mashariki ya kati yanayohusika katika mzozo nchini Yemen, Misri, Saudi Arabia na Umoja wa falme za Kiarabu.
Ripoti hiyo inakuja wakati mgumu wa matatizo kwa serikali ya Ujerumani , huku kukiwa na kelele zilizozushwa na picha ya vifaru vilivyoundwa Ujerumani vikipelekwa nchini Syria na majeshi ya Uturuki. Hali hiyo pia inaleta shaka kuhusu mazungumzo ya hivi karibuni kati ya chama cha CDU na SPD kuhusu kuunda serikali ijayo ya Ujerumani, ambayo pia inajumuisha ahadi ya kuweka sheria kali kuhusiana na mauzo ya silaha.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman